Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ugonjwa kipindupindu tishio Malawi, Tanzania yajipanga

Muktasari:

  • Katika kipindi cha siku 14 zilizopita tangu juzi, mikoa 14 nchini Malawi iliripoti matukio ya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu, huku takwimu za jumla zikionyesha mikoa 29 ikirekodiwa kuwa na ugonjwa huo.

Dar/Mbeya. Wakati ugonjwa wa kipindupindu ukikatisha maisha ya wananchi 661 nchini Malawi, Wizara ya Afya nchini imetuma timu ya wataalamu 11 katika mikoa ya Songwe, Mbeya na Ruvuma kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya nchini Malawi, hadi Januari 5, mwaka huu, jumla ya watu 19,629 wameambukizwa ugonjwa huo, huku watu 442 wakiruhusiwa kutoka hospitali na 905 wakiwa bado wanapatiwa huduma hospitalini nchini humo.

Katika kipindi cha siku 14 zilizopita tangu juzi, mikoa 14 nchini Malawi iliripoti matukio ya maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu, huku takwimu za jumla zikionyesha mikoa 29 ikirekodiwa kuwa na ugonjwa huo.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Afya, Said Makora alisema wizara hiyo tayari imetuma madaktari, wataalamu wa magonjwa ya mlipuko pamoja na maofisa afya mazingira katika mikoa hiyo kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

“Hatuna mgonjwa, tulipata kesi moja Novemba mwaka jana na mgonjwa alitibiwa akapona, baada ya hapo tuliwatuma wataalamu kwenye mikoa iliyopakana na nchi ya Malawi, yaani Wilaya ya Ileje (Songwe), Mbambabey (Ruvuma) na Kyela (Mbeya). Wataalamu hao walikwenda kuzijengea uwezo kamati za afya za mikoa na wilaya.

“Kamati hizo zilijengewa uwezo wa kutambua ugonjwa kupitia vipimo vya haraka, kuboresha mfumo wa utoaji taarifa endapo kutakuwa na kesi za ugonjwa,” alisema.

Makora aliongeza kuwa, “maofisa afya walijengewa uwezo katika kutoa elimu kwa wananchi huko mipakani namna ya kuzingatia usafi wa mazingira na uhifadhi wa vyakula na unawaji wa mikono na kufanya vikao vya ujirani mwema na watu wa Malawi, lengo kuweka utaratibu wa watu wanaovuka mipaka wanafuata kanuni za afya.”

Akizungumzia ushirikiano wa wizara na mamlaka nyingine, Makora alisema wanashirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wananchi wanafuata taratibu za afya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu.

Mbali na hayo, Makora alisema wanashirikiana na mamlaka za maji za wilaya, hususani Wilaya ya Kyela na Ileje zilizokuwa na changamoto ya maji safi na salama ambazo zimewezesha upatikanaji wa maji baada ya mlipuko wa ugonjwa huo.

“Pia tuna utaratibu wa kubadilishana taarifa ya hali na mwenendo wa kupambana na ugonjwa wa kipindupindu nchini Malawi. Kwa upande wetu hali iko shwari,” alisema.

Akieleza mikakati ya Mkoa wa Mbeya kukabiliana na ugonjwa huo, mkuu wa mkoa huo, Juma Homera aliwaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri zinazopakana na Malawi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia suala la usafi.

“Nimetoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya, maofisa afya na wakurugenzi suala la usafi lipewe kipaumbele. Iwe ajenda ya kudumu na eneo ambalo litaripotiwa kuwa na mgonjwa wa kipindupindu uongozi utawajibishwa,” alisema.

Mfanyabiashara Tukuswiga Jolam alisema Serikali ichukue tahadhari ya ugonjwa huo kwa wilaya ambazo zimepakana na nchi ya Malawi, hasa Wilaya za Kyela na Ileje.

“Tahadhari isipochukuliwa kuna hatari kubwa ya ugonjwa huo kuingia nchini kutokana na muingiliano wa shughuli za kiuchumi kati ya nchi jirani ya Malawi na Tanzania,” alisema.


Usafi upewe kipaumbele

Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM) na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kuna kila sababu suala la usafi kupewa kipaumbele kwa uongozi wa jiji na si kusubiri viongozi watoe maelekezo.

“Sidhani kama inaleta afya sisi viongozi kukemea suala la usafi wakati wakurugenzi, maofisa mazingira, wenyeviti wa Serikali za mitaa wapo, sasa utafika wakati ni lazima tuanze kuwajibishana,” alisema.


Kuhusu Kipindupindu

Kipindupindu ni ugonjwa unaotokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binadamu uletwao na vimelea vya bakteria ambao hufahamika kitaalamu kama ‘Vibrio cholerae’.

Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine na usipo tibiwa kwa haraka, mwathirika hupoteza maisha ndani ya saa chache.

Mtu huambukizwa kipindupindu kutokana na uchafu, hasa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya ugonjwa huo.


Dalili za ugonjwa

Dalili za ugonjwa wa kipindupindu ni kuharisha ghafla choo chenye majimaji (ambacho rangi yake ni kama maji ya mchele) na chenye harufu mbaya kama shombo ya samaki, kutapika pamoja na kupungukiwa maji mwilini.


Jinsi ya kuzuia kipindupindu

Miongoni mwa njia zinazofaa katika kuzuia milipuko ya ugonjwa huo ni kutumia maji safi na salama, hasa kwa kuhakikisha yanachemshwa na kuchujwa kabla ya kunywa.

Kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka chooni na kabla ya kula, kufunika chakula kikiwa mezani, ili nzi wasitue juu yake pamoja na kujenga choo umbali wa angalau mita 30 kutoka chanzo cha maji.

Kutokana na msimu huu kuwa wa maembe, matunda ambayo huwa ni kichocheo kimojawapo cha vimelea vya ugonjwa huo, ni muhimu kusafisha matunda hayo na kuyamenya kabla ya kuyatumia.

Pia ni vema kwa wanaotumia maziwa yatokanayo na wanyama kuhakikisha wanayachemsha kabla ya kuyatumia na kuepuka kutumia nyama au samaki ambao hawajapikwa vizuri.