Tuache kauli za ukatili, dharau kwa wauguzi

Muktasari:
- Kila ifikapo Mei 12 ya kila mwaka, wauguzi kote duniani huadhimisha siku yao na kwa Mkoa wa Njombe, wameadhimisha leo.
Njombe. Jamii imetakiwa kuwaheshimu na kuwathamini wauguzi kama kundi muhimu linalochukua nafasi ya kipekee katika uhai na mfumo wa afya kwa kuepuka vitendo vya ukatili wa maneno, dharau na lawama zisizo na msingi.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Mei 13, 2025 na wauguzi mkoani Njombe wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani ambayo imefanyika wilaya ya Njombe.
Muuguzi kutoka kituo cha afya Njombe, Felista Lova amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuboresha mazingira ya kazi, bado baadhi ya wananchi wamekuwa chanzo cha kuharibu morali ya wahudumu hao kwa kukosa ushirikiano na kuwabeza hadharani.
Amesema wahudumu wengi wanajitahidi kutoa huduma bora licha ya changamoto za vifaa na mzigo mkubwa wa kazi.
“Lakini vitendo vya kudhalilishwa na tunaowahudumia kunatuvunja moyo na kuna athiri utendaji wetu wa kazi,” amesema Lova.
Hata hivyo, muuguzi huyo amesema anafarijika kuona anapokuwa kazini na kukutana na mgonjwa akamuhudumia na kupona, inampa nguvu ya kuendelea na kazi hiyo kwa uadilifu.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha wauguzi Mkoa wa Njombe, Raphael Kalulu amesema ni vigumu kwa wauguzi kuwa viongozi wa mageuzi katika sekta ya afya kama mazingira ya kazi hayatapewa kipaumbele.
Amesema mageuzi hayo yanatakiwa kwenda sambamba kwa kurejeshwa kwa heshima ya wauguzi ndani ya jamii ambayo imekuwa ikiwatumikia kwa moyo na uadilifu.
"Tunahimiza Serikali kuongeza wauguzi na motisha ili nguvu ya mabadiliko iweze kuonekana kwa pande zote,” amesema Kalulu.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Mkoa wa Njombe, Dk Mashaka Kisulila amewataka wauguzi kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi ili imani kwa wananchi iweze kurejea.
"Nawaomba ndugu zangu wauguzi muendelee kupiga kazi kwa haya mengine mnayoyasikia muyapuuzie kwa sababu kazi ndiyo itakutambulisha,” amesema Dk Kisulila.
Mganga wa Halmashauri ya mji wa Njombe, Dk Jabir Juma ametoa wito kwa wananchi mkoani humo kushirikiana na wauguzi badala ya kuwa chanzo cha taharuki na kuleta migongano.
"Pale ambapo wanawashukuru wauguzi na kutambua kazi zao muuguzi anapata imani na kujua huduma anazotoa ni bora," amesema Dk Juma.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Njombe, Lilian Nyemele amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya kazi kwa wauguzi sambamba na kuwashirikisha kikamilifu katika maamuzi muhimu ya kisekta.
"Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuthamini sekta ya afya kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma na vifaatiba" amesema Nyemele.