Uchunguzi wa Takukuru Arusha wabaini watumishi wawili kughushi nyaraka

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo
Muktasari:
- Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Mkoa wa Arusha, inafanya uchunguzi wa mfumo mzima wa malipo ili kubaini kampuni hewa na namba bandia za mlipakodi
Arusha. Tuhuma za kughushi nyaraka, uchepushaji wa makusanyo ya Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma, zimechukua sura mpya baada ya watumishi wawili kudaiwa kuhusika kutengeneza namba bandia ya mlipakodi na kampuni hewa ya kulipia makusanyo hayo.
Kutokana na uchunguzi huo wa awali kubainisha hilo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha, inafanya uchunguzi wa mfumo mzima wa malipo ili kubaini kampuni nyingine hewa na namba bandia za mlipakodi zilizotumika kuchepusha kodi au mapato yoyote katika halmashauri hiyo.
Takukuru imefanya uchunguzi huo ikiwa ni agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kufuatia tuhuma zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo kudai kulipa kodi ya huduma Sh24 milioni, lakini akapewa risiti ya Sh3.6 milioni.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Mei 26, 2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema uchunguzi wa awali umebaini watumishi wawili wa halmashauri hiyo wamehusika kughushi nyaraka ikiwamo kutengeneza namba bandia ya mlipakodi na kutumia kampuni hewa kulipia mapato.
“Uchunguzi kwa sasa uko juu ya watumishi wawili, mmoja tumebaini ndiye aliyetengeneza namba bandia ya mlipakodi na mwingine kampuni hewa ya kulipia makusanyo, tunaendelea na uchunguzi ili kubaini kuna kitu kinaweza kusababisha ubadhirifu,” amesema Ngailo.
“Tunaona bado kuna udhaifu mkubwa kama anayetengeneza namba ya mlipakodi, mwingine anaweza kutengeneza kampuni hewa ambayo inatumika kukusanya kodi itakuwa shida, tunaendelea na uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma ikiwamo za matumizi mabaya ya madaraka. Kwa hiyo, tutaangalia mfumo mzima kukagua tuone, je, hawa kina The Tanganyika Wilderness Camps wa aina hiyo wako wangapi? amehoji.
Mei 22, alieleza kuwa wamehoji watumishi saba wa jiji hilo wakiwamo kutoka kitengo cha ukusanyaji wa mapato.
Katika kikao cha awali cha wadau wa utalii, Chambulo aliibua tuhuma hizo ikiwamo utengenezaji wa nyaraka bandia na kuchepusha baadhi ya makusanyo ya kodi, lililomlazimu Makonda kuagiza uchunguzi wa Takukuru.
Katika kikao hicho, Chambulo alionyesha nyaraka alizodai zinathibitisha matendo maovu ya watendaji wa jiji hilo na kuwa hata utambulisho wa biashara inayoonekana katika fomu hiyo imejazwa tofauti na ya kampuni yake.
Katika ukurasa wa kwanza wa fomu aliyopewa na halmashauri hiyo, Chambulo alidai imeandikwa jina la kampuni yake, lakini namba za biashara na utambulisho siyo zake.
“Hii nyaraka siyo ya kwangu, nyaraka niliyojaza ni hii hapa na mhuri wangu nimepiga, alipata wapi jina linaitwa The Tanganyika Wilderness Camps, ukifungua hapa kwenye nyaraka ya halmashauri (anaonyesha).
“Ukiangalia vizuri namba ya mlipaji, hii siyo hata namba ya kwetu, hata tarakimu za simu zimepungua moja, kwa hiyo imebandikwa, yangu hii hapa (akionyesha fomu hizo),” alidai Chambulo.