‘Tusiongeze programu kwa kasi’

Muktasari:
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kujikita katika vitivo vya kilimo na teknolojia ili kutoa umahiri uliokusudiwa.
Butiama. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia kujikita katika vitivo vya kilimo na teknolojia ili kutoa umahiri uliokusudiwa.
Akizungumza na uongozi na watumishi wa chuo hicho Julai 6, 2023 kwenye Kampasi ya Oswald Mang'ombe Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewataka kutokuwa na programu nyingi ambazo zinaweza kuondoa ufanisi na ubora.
“Tusijaribu kwenda na mambo mengii, tungependa hichi chuo kiwe alama inayotambulika kimataifa, kwahiyo ningependa tusiongeze programu kwa kasi kubwa,
“Yapo mambo mengine ambayo yanaweza kuwa sio kilimo lakini yanahusiana kama Tehama hata biashara lakini mkaweka vizuri,” amesema Profesa Mkenda
Waziri huyo aliyekagua na kutembelea miundombinu ya chuo hicho kabla ya kuzungumza na watumishi amesema ameridhishwa na maandalizi ya ukarabati wa chuo hicho kinachotarajia kudahili wanafunzi Novemba mwaka huu baada ya kutodahili kwa miaka 10 tangu kianzishwe 2014.
"Tumezunguka kote, tumekagua na kwakweli tumeridhika na nina imani kwamba tukienda hivi basi tutakua tayari kupokea wanafunzi kwa ajili ya masomo ndani ya mwaka huu wa masomo,”amesema
Profesa Mkenda amewaambia watumishi wa chuo hicho tayari wajumbe wa baraza la chuo wameshapatikana ambapo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda ndiye mkuu wa chuo hicho.
Akitoa taarifa ya ukarabati, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Lesakit Mellau amesema tayari wamepokea Sh1 bilioni kati ya Sh2. 66 bilioni zilizotengwa na Serikali kupitia wizara hiyo kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na ujenzi wa bweni chuoni hapo.
Fedha hizo zitajenga mabweni matatu, jengo la maabara ya baiolojia, ofisi ya walimu na ukarabati wa majengo na miundombinu.
“Katika zoezi la ukarabati tumezishirikisha taasisi za wenzetu kama vile VETA, TBA, Bonde la Ziwa Victoria, Halmashauri ya wilaya ya Butiama na Ruwasa ambao wametuhakikisha kuwa tutapata maji ya kutosha kuhudumia chuo hiki,”amesema
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda ameihakikishia wizara hiyo kukarabatiwa na kuwa chuo cha mfano nchini ili kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambacho pia kitachochea ubunifu, umahiri katika sekta ya kilimo na hata Utalii katika ukanda huo.
Naye, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ametoa rai kwa uongozi wa chuo hicho kuhakikisha ukarabati unaanza mara moja na kwa ubunifu.
Baada ya mazungumzo na watumishi, Profesa Mkenda alifika kwenye kijiji cha Rwamkoma na kukagua eneo Maalum ambalo itajengwa miundombinu ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere tawi la Butiama ambapo zaidi ya Sh44.5 bilioni zitatumika chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.