Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Amani ya nchi imo mikononi mwa vyombo vya habari’

Muktasari:

  • Wadau wa sekta za habari wamekutana katika kongamano la kujadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Dar es Salaam. Wadau wa habari wamesema ili nchi ya Tanzania iendelee kuwa na amani na utulivu, vyombo vya habari vina jukumu la kulinda hali hiyo kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Mwaka huu Tanzania, itafanya uchaguzi mkuu utakaowaweka madarakani Rais, wabunge na madiwani kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Hayo yamesemwa katika kongamano wadau wa kujadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, lililofanyika leo Jumatano, Julai 9, 2025 jijini Dar es Salaam. 

Miongoni mwa wadau ni viongozi wa dini, wanahabari, wahariri na polisi wa mikoa (RPC) yote nchini, wakuu wa vikosi vya polisi. Kongamano hilo  limefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Dk Biteko amewataka waandishi wa habari kuhimiza uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa watu kuheshimu maoni na mtazamo wa wengine,"hata kama hukubaliani nayo, lakini kuna dogo la maana la kuchukua."

Dk Biteko amesema mtu yeyote anayeweza kudhani unaweza kufanya kazi bila vyombo vya habari anajidanganya.

"Muhimu hapa tusivilaumu vyombo vya habari bali tuvipe taarifa rasmi ili vihabarishe jamii."

Akijenga hoja kuelekea uchaguzi huo, Dk Biteko amesema: "Tuhimize maelewano, uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa kuheshimu maoni, mtu kuheshimu mtazamo wa mtu mwingine."

Ametolea mfano, anayeamini Yanga ni timu bora, aheshimiwe sawa na yule anayesema Simba ni timu bora.

"Hata kama mtu anasema jambo hulipendi, msikilize kwani kuna jambo dogo zuri lichukue," amesema Dk Biteko.

Akitoa mada kwenye mkutano huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesisitiza uzalendo kama silaha ya kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Profesa Kabudi amesisitiza umoja na mshikamano wa Taifa unategemea uzalendo wa makundi yote nchini yakiongozwa na vyombo vya habari.

"Mataifa mengi duniani yameundwa na jamii zenye asilimia moja, sisi Watanzania tuna makabila yenye asili tofauti kuliko nchi yoyote duniani, hata hivyo ni uzalendo uliojengwa mioyoni mwa Watanzania ndio umetufikisha hapa," amesema Kabudi.

Amebainisha kuwa, Tanzania ni nchi iliyozaliwa na kujengwa katika misingi umoja, mshikamano kwa kuvunja mipaka ya makabila kupitia lugha ya Kiswahili.

"Uzalendo ni kuyaacha yale unayoyaamini wewe pekee na kufuata yale ambayo Taifa linamasilahi,” amesema.

Kuhusu nafasi ya vyombo vya habari, Profesa Kabudi ambaye kitaalamu ni mwandishi wa habari na mwanasheria, amesema ubia wa vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi nchini ni suala la msingi katika kuendeleza na kudumisha umoja na amani ya Taifa.

"Jukumu la kusimamia amani ni la vyombo vya ulinzi na usalama huku vyombo vya habari vikiwa na jukumu la kutoa taarifa kwa umma, hivyo ni muhimu vyombo hivi kushirikiana ili kuweka mazingira ya usawa na umoja wa kitaifa,” amesema.

Akizungumzia wajibu wa Jeshi la Polisi katika Usimamizi wa Ulinzi na Usalama, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema wajibu wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha uwepo wa mazingira rafiki ya haki na kiusalama wakati wote wa uchaguzi ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.

Kuhusu vyombo vya habari, Misime ametoa wito kwa waandishi wa habari kuepuka vichwa vya habari vya uchochezi huku akisisitiza ushirikiano wa waandishi wa habari na jeshi hilo.

"Waandishi wa habari wanapaswa kuacha habari za kichochezi na habari ziwe katika usawa ili kulinda amani na umoja," amesema.

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC-UDSM), Dk Egbert Mkoko ametahadharisha vyombo vya habari visipofanya kazi kwa misingi ya kitaaluma ni weledi inaweza kusababisha mgawanyiko katika jamii.

Akitoa mwongozo kwa vyombo vya habari katika kuripoti Uchaguzi Mkuu wa 2025, Dk  Mkoko amezitaka mamlaka za habari nchini zikiwamo, Bodi ya Ithibati, Habari Maelezo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wandishi wa habari na vyombo vya habari kuzingatia maadili ya kitaaluma kwa kutimiza wajibu wake ipasavyo ili kulinda amani na moja wa kitaifa.

"Mamlaka za habari nchini zinawajibu wa moja kwa moja, pamoja na mamlaka za uchaguzi zikiwamo za Jeshi la Polisi, Tume Huru ya Uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea,  kuzingatia unyeti wa suala la uchaguzi hasa kutoa mazingira ya haki na usawa katika kushughulika na masuala ya uchaguzi," amesema.

Akitaja mikakati inayochukuliwa na mamlaka za vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Serikali kupitia Bodi ya Ithibati ina wajibu wa kusimamia mfumo wa utambuzi na usajili wa wanahabari wote nchini kidigitali ili kuhakikisha watu wasio na taaluma ya uandishi wa habari hawafanyi kazi hiyo.

"Tunasajili na kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari, mpaka sasa, zaidi ya wanahabari 2,900 wamesajiliwa na Bodi ya Ithibati," amesema.

Msigwa, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa,  uandishi wa habari unapaswa kufanywa kwa kuzingatia maadili ili kulinda umoja na amani katika jamii.

Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka amesema vyombo vya habari vinapaswa kuepuka habari za kuchochea chuki na mgawanyiko katika jamii ili kulinda amani na umoja wa kitaifa.

"Uandishi wa habari uzingatie usawa, uepuke habari za kugawa na kupendelea ili kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa" amesema.

Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe amesisitiza kuwa, suala la amani linapaswa kuzingatiwa na kila chombo cha habari nchini.

Amesema kama kila chombo kitazingatia, basi ushiriki wa wanawake katika uchaguzi wa mwaka huu utakuwa kikamilifu.

"Hata wanahabari wanawake tunahitaji mazingira ya amani ili kushiriki kikamilifu, hivyo ni vyema kuimarishwa kwa suala la ulinzi na usalama ili kuwezesha ushiriki wa kundi hili vyema," amesema.