‘Sheria ya Makosa ya Mitandao imewapa mamlaka makubwa Polisi’
Muktasari:
Muungano wa Haki ya Kupata Habari (CORI), umesema kifungu cha nane cha sheria ya Mkosa ya Mitandao kinamruhusu inspekta msaidizi wa polisi, kukagua au kushikilia kifaa chochote alichokikamata.
Dar es Salaam. Mjumbe wa Muungano wa Haki ya Kupata Habari (CORI), James Marenga amesema Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015 imelipa Jeshi la Polisi mamlaka makubwa, hivyo inapaswa kufanyiwa marekebisho ili isilete madhara.
Marenga amebainisha hayo leo Oktoba 20, 2022 wakati wa warsha maalumu iliyoandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa lengo la kuhamasisha marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya habari.
Amesema sheria hiyo ina vifungu mbalimbali ambavyo vina utata na vinahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuondoa kadhia inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Amesema kifungu cha nane cha sheria hiyo kinamruhusu inspekta msaidizi wa polisi, kukagua au kushikilia kifaa chochote alichokikamata.
"Sheria hii inatoa mamlaka makubwa kwa polisi, tukiiacha hivyo ilivyo italeta madhara makubwa wakati wa utekelezaji wake," amesema Marenga ambaye pia ni wakili wa kujitegemea.
Marenga amesema kuna haja ya kuiga kwa mataifa mengine ambayo yana utaratibu mzuri ambapo ofisa wa polisi haruhusiwi kukagua nyumba au ofisi ya mtu bila kuwa na kibali cha Mahakama.
Ametokelea mfano nchi za Ghana na Zambia ambazo zina utaratibu huo huku akisisitiza itasaidia kulinda haki ya mtuhumiwa wakati wa utekelezaji wa sheria hiyo.
Marenga amebainisha pia kifungu cha 50 cha sheria hiyo hakitoi haki ya mtu kukata rufaa. Pia, amesema kifungu cha 38 kinabainisha kwamba usikilizaji wa shauri la mtu utafanyika hata bila mhusika kuwepo.