Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Msiingilie mchakato uboreshaji daftari la kuduma la mpigakura’

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi Stephen Elisante akitoa elimu kwa wadau wa uchaguzi mkoani hapa.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Tume Huru ya Uchaguzi, Mtibora Selemani, kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za uchaguzi.

Njombe. Mawakala na viongozi wa vyama vya siasa wametakiwa kuzingatia sheria kwa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwenye vituo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Tume Huru ya Uchaguzi, Mtibora Selemani, kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za uchaguzi.

Akizungumza leo Jumatano Januari Mosi, 2025 katika mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Njombe, Selemani amesema iwapo kutatokea changamoto wakati wa uboreshaji, zinapaswa kushughulikiwa kupitia taratibu zilizowekwa kisheria au kuwasilishwa rasmi kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.

Selemani amesisitiza kuwa tume itaendelea kuzingatia Katiba, sheria za uchaguzi pamoja na kanuni zilizotungwa chini ya sheria hizo katika uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura.

"Nawaomba viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, na maelekezo ya tume ili kuhakikisha kuwa mchakato wa uboreshaji unafanyika kwa amani na kwa mujibu wa taratibu," amesema Selemani.

Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Uchaguzi, Stephen Elisante, amesema Mkoa wa Njombe una wakazi zaidi ya laki nane, na tume inatarajia kuandikisha watu 80,994 kwenye daftari hilo.

Amewataka wananchi kutumia fursa hiyo adimu ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

"Tutumie fursa hii kujiandikisha na kuboresha taarifa zetu ili kila mmoja awe na haki ya kushiriki uchaguzi mkuu," amesema Elisante.

Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo, Ally Mhagama amesema baadhi ya malalamiko ya vyama vya upinzani, kama vile ushiriki wa watu walioko magerezani kwenye mchakato wa uchaguzi, tayari yamefanyiwa kazi na tume.

"Hata hivyo, tunahitaji kuona utekelezaji wa mabadiliko haya kivitendo, badala ya uteuzi wa walimu au watendaji wanaoweza kuwa na miegemeo ya kisiasa," amesema Mhagama.

Naye Katibu wa Mafunzo, Siasa, na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, Josaya Luoga amewasihi wanachama wa chama hicho kutoingilia michakato ya uchaguzi kwa kuwa tume ipo kisheria.

Baadhi ya wananchi, akiwemo Neema Shukuru, wameeleza dhamira yao ya kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa ni kutaka kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

"Nawashukuru tume kwa kuja hapa Njombe. Tunaahidi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili tuweze kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi wetu," amesema Shukuru.