‘Mnaoenda kuhiji tazameni fursa ya biashara Saudi Arabia’

Katibu wa baraza la Ulamaa Bakwata Taifa,Sheikh Mussa Hemed akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu waaslamu watakaoenda safari ya Hijja. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Baraza Kuu la Kiislamu nchini, (BAKWATA), leo limekabidhi vyeti vya uthibitisho kwa taasisi 24 zilizokidhi vigezo vya kuwapeleka Mahujaji wa Kitanzania nchini Saudi Arabia Juni Mwakani. Mbali na zoezi la ugawaji vyeti pia taaisisi hizo zimeaswa juu ya mambo mawili.
Dar es Saalam. Taasisi 24 zilizokidhi vigezo kuwasimamia Watanzania katika safari ya Hijja zimetakiwa pia kuangalia fursa nyingine za kibiashara nchini Saudi Arabia.
Wakizungumza wajumbe wa Baraza Kuu la Kiislamu nchini (Bakwata), mbele ya wawakilishi wa taasisi hizo zilizokidhi vigezo leo Jumapili Novemba 19, 2023 jijini Dar es Salaam, wamesema mbali na kufanya ibada nchini Saudi Arabia pia kuna uwezekano mkubwa wa kufanya biashara kama mataifa mengine yanavyofanya.
"Kwanini na sisi Watanzania tusifanye biashara tunapoenda kwenye ibada ya Hijja, tunakwama wapi? Wenzetu Wanaijeria na mataifa mengine wanafanya biashara," amehoji Sheikh Ali Ngeruko wakati wakikabidhi vyeti kwa taasisi hizo.
Sheikh Ngeruko ambaye ni Naibu Kadhi Mkuu amesema Watanzania wanaweza kwenda kama wamachinga kupeleka bidhaa mbalimbali nchini humo.
"Ifike wakati tuelimishane biashara ni ibada na Hijja ni soko na soko hili sisi tunalipoteza. Kwanini kama Watanzania hatuonekani kwenye ramani ya soko la Saudia. Lile soko lina baraka wito wangu tuwaongoze Watanzania kama wamachinga.
"Tukisema tukumbatie dhana kwamba ukienda kuhiji hauruhusiwi kufanya biashara lakini wenzetu wanaenda wananufaika," amesema.
Wakati Sheikh Ngeruko akiasa kuhusu biashara, kwa upande wake Sheikh Ali Muhidin amegusia kuhusu matumizi ya simu wakati wa ibada huko Makka.
Amesema suala la kujirekodi wakati ibada si jambo zuri na halipendezi hivyo taasisi zinapaswa kuwasimamia Mahujaji kutofanya hivyo wanapokuwa wapo ibadani.
"Sasa hivi simu hizi zimekuwa kama mtindo mtu amekaa hapa anajirusha mtandaoni ili iweje? au anauliza mbona hunipigi picha, kwani pale umeenda kupiga picha. Wewe pale umefuata ibada. Lazima ujue umekwenda nyumba tukufu na ina heshima zake," amesema.
Kadhalika, amesema ndio maana zinawekwa semina ili watu watambue wanaenda mji gani. Hivyo taaisisi ziwafahamishe waelewe juu ya utukufu wa Hijja.
Naye, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje Bakwata, Tahir Al-Mussawa amesema Wizara ya Hijja ya Saudia imetoa nafasi ya Watanzania 25,000 ila kama Tanzania wameomba Mahujaji 3,700 kutokana na uchache wa mahujaji.
"Tunatumaini tunavyozidi kwenda Mahujaji nao wataongezeka ukiangalia mara ya mwisho walikuwa 3,100 hivyo idadi inapanda na tunaraji tutafikia idadi hiyo iliyotolewa na Saudia," amesema.
Akizungumzia kuhusu waliyoambiwa na Bakwata, mmoja wa wawakilishi wa taasisi hizo Kassim Abdallah kutoka taasisi ya Musafir Hajir and Umrah amesema suala la biashara linawezekana kwakuwa kuna watu wanaofanya hivyo.
"Kuna watu toka enzi za Mtume walikuwa wanapeleka bidhaa au kuzinunua kurudisha nchini mwao, sio tu walikuwa wanaenda kwa ajili ya jambo moja. Hata sisi tunaweza kupeleka viungo, vyakula, " amesema Abdallah alipokuwa akohojiwa na Mwananchi.
Pia, amesema suala la kuzingatia taratibu na sheria za nchi ya Saudia kuwa wanafanya nini ili isiwe kuuza kiholela.
Vilevile kuhusu matumizi ya simu amesema inatia shaka nia ya hujaji kuwa ameenda kwaajili ya ibada au kwaajili ya simu.