Miili 36 ya ajali ya Same ilivyoagwa KCMC

Muktasari:
- Shughuli ya kuaga miili hiyo imefanyika leo Alhamisi Julai 3, 2025 kwenye viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) mjini Moshi
Moshi. Ni siku iliyojaa huzuni na majonzi wakati familia za watu 36 kati ya 42 zikiaga miili ya wapendwa wao waliofariki dunia katika ajali ya magari mawili ya abiria wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Shughuli ya kuaga miili hiyo imefanyika leo Alhamisi Julai 3, 2025 kwenye viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) mjini Moshi.
Ajali hiyo, iliyotokea Juni 28, 2025 eneo la Sabasaba, Same mjini, ilihusisha basi kubwa la Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Same kwenda Moshi.
Magari hayo yaligongana uso kwa uso kisha kuwaka moto yakiwa na abiria ndani, hali iliyosababisha vifo vya watu 42.
Katika basi dogo aina ya Toyota Coaster walifariki watu 31, waliokuwa wakielekea kwenye sherehe ya harusi mjini Moshi, huku kwenye basi la Chanel One wakiaga dunia watu 11.
Leo asubuhi, umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki ulifurika katika Hospitali ya KCMC kuaga miili ya wapendwa wao.
Majeneza yaliyobeba miili hiyo ilipowasili kwa magari ya polisi na kushushwa kwenye viunga vya hospitali hiyo, vilio na simanzi vilitawala huku baadhi ya watu wakishindwa kabisa kujizuia.
Shughuli hiyo ya kuaga imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na viongozi wengine wa Serikali na chama.
Baada ya ibada maalumu ya kuwaombea marehemu, miili ilikabidhiwa kwa familia na kuanza safari kuelekea wilayani Same kwa ajili ya mazishi.
Babu amesema Serikali imetoa ubani wa Sh126 milioni huku kila familia ikikabidhiwa Sh3 milioni kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya mazishi.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo maalumu, mmoja wa wawakilishi wa wafiwa, Kapteni Farijalla Mkojera, amesema: “Msiba huu haufutiki mioyoni mwetu na kwenye akili zetu, lakini kwa jinsi mlivyotukimbilia na kuwa na sisi, tunajihisi ni Watanzania na tuna ndugu. Tunashukuru sana Serikali kwa jinsi ilivyotusimamia na kutusaidia kufanikisha jambo hili.”
Amemuomba mkuu wa mkoa huyo awafikishie salamu za asante kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa namna alivyoshirikiana nao katika kipindi hiki cha majonzi.
“Najua na yeye ameondokewa na Watanzania wenzake na nguvu kazi ya Taifa, lakini watumishi wengi wa Serikali pia wamehangaika usiku na mchana kuhakikisha mambo yanaenda kwa utaratibu kama alivyowaagiza, tunasema asante sana,” amesema mwanafamilia huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akizungumza huku akibubujikwa machozi amesema: “Tumepata pigo kubwa sana. Mimi kama mkuu wa wilaya nilikuwa nashindwa hata kupita mjini kwa sababu kila mtaa umepatwa na msiba huu. Wengi ni watu ninaowafahamu kwa sura, nimeumia sana. Japokuwa nina maumivu makubwa, ninamshukuru sana mkuu wa mkoa kwa ushirikiano wake.”
Mkuu wa Mkoa Babu amesema: “Tumepata msiba mkubwa sana. Hakuna maneno ya kueleza kwa undani, uchungu na maumivu haya. Tumepoteza watoto, wake, waume, wajomba, marafiki. Kila mmoja wetu anaweza kuelewa maumivu ya kumpoteza mpendwa wake. Kwa niaba ya mkoa, natoa pole nyingi na kumuomba Mungu awatie nguvu na uvumilivu wafiwa wote.”
Pia, aliyekuwa Mbunge wa Same Magharibi, David Mathayo ametoa salamu zake za rambirambi huku akisema katika jimbo lao pekee, watu 33 wamefariki dunia kutoka kata mbalimbali.
"Ndugu waombolezaji katika jimbo langu wamefariki watu 33 kutoka katika kata mbalimbali, huu ni msiba mkubwa sana ambao umetokea katika jimbo letu," amesema Mathayo.
Hata hivyo, katika ibada hiyo maalumu ya kuaga ipo nyumba iliyopoteza watu 10, wakiwamo wanafamilia wanne na wapangaji sita ambao pia wameagwa katika viwanja hivyo.