Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Michezo ya watoto inachochea makuzi ya ubongo’

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Joel Mwakapala akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi Jumuishi wa Taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) mkoani Mwanza. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Wazazi na walezi wameshauriwa kutenga muda wa watoto kucheza ili kusaidia kujenga muunganiko wa seli na kuchochea makuzi ya ubongo.

Mwanza. Michezo kwa watoto kati ya umri sifuri hadi miaka nane imetajwa kusaidia kujenga muunganiko wa seli na kuchochea makuzi ya ubongo.

Wakizungumza Septemba 22, 2023 wakati wa uzinduzi wa Mradi Jumuishi wa Taifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT- MMMAM) jijini Mwanza, wadau wa makuzi ya watoto wamesema michezo ina msaada mkubwa kwa mtoto kufikia utimilifu wake.

"Tuna wahimiza wazazi na walezi kuwatengea muda wa kutosha wa kucheza kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwanunulia vifaa vya kuchezea mazingira ya nyumbani kwa sababu inachochea makuzi ya ubongo wao," amesema Andrew Nkunga, Ofisa Mawasiliano na Ushirikiano kutoka Shirika la Early Childhood Development Network (TECDEN)

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Watoto duniani (Unicef) kwa kushirikiana na Shirika la Afya duniani (WHO) umeonyesha umri sahihi wa kuwekeza kwa mtoto ni kati ya mwaka sifuri hadi nane wakati ambapo ubongo hukua kwa asilimia 90 hadi kufikia utimilifu wake.

Katika utafiti huo mambo matano yamependekezwa ili kufikia utimilifu huo ambayo ni afya bora, lishe bora, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama kwa watoto.

Akizungumzia mradi huo unaotarajia kutumia zaidi ya Sh941 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Joel Mwakapala amesema kushindwa kuwekeza katika umri huo itawalazimu kutumia gharama kubwa  ukubwani.

"Tuna amini hayo mambo yote matano mtoto akiyapata kwa wakati mmoja itamsaidia yeye kufikia utimilifu wake kwa sababu Sayansi inasema ili taifa liweze kufikia malengo makubwa lazima uwekezaji mkubwa ufanyike kwa watoto wakiwa bado wadogo kwani tukichelewa tukawekeza akiwa mkubwa Serikali na wadau watalazimika kutumia gharama nyingi," amesema Mwakapala

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mratibu wa Mradi huo mkoani humo, Janeth Shishila ameongeza kuwa chanzo cha mmonyoko wa maadili katika jamii ni matokeo ya wazazi kushindwa kuwekeza kwa watoto katika umri huo.

"Tunasema katika jamii kuna mmonyoko wa maadili lakini kumbe haukuanza akiwa kijana ulianza akiwa mtoto sasa wito wangu kwa jamii, viongozi wa dini na familia kuchukua jukumu la kulea na kuwa karibu na watoto wao kuanzia yule aliye tumboni hivyo hivyo kwa viongozi wa dini walio katika nafasi kubwa ya kutoa elimu sio imani tu na hata katika malezi," amesema Shishila

Akizindua mradi huo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana ametoa wito kwa viongozi wa ngazi ya mkoa hadi Kata kwenda kuutekeleza huku, akiwasihi wazazi kuwalea wototo katika misingi bora kwa ajili ya kulitumikia taifa.

"Sisi kama Mwanza sio kwamba tumechelewa kuzindua na kuanza kutekelez hapana! tuliashanza kutekeleza rasmi ni kwamba tumezindua na kila mmoja wetu achukue majukumu yake na kuyafanyia kazi kuhakikisha inatekelezwa  na kwamba watoto wetu wakue kwa misingi bora kwa ajili ya kulitumikia taifa lao," amesema Elikana