Makalla aeleza safari yake CCM, changamoto iliyomkabili Mwanza

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo Amos Makalla (kulìa) akimkabidhi kitabu chenye kero mbalimbali za wakazi wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo Said Mtanda (kushoto) katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika leo Aprili 6, 2024 mkoani Mwanza. Picha na Anania Kajuni
Muktasari:
Makalla amesema alipoteuliwa kushika nafasi ya ukuu wa Mkoa wa Mwanza Mei 15, 2023 alianza kutumiwa ujumbe mfupi kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, kila ujumbe ukimtaka ashugulikie Uwanja wa Ndege wa Mwanza
Mwanza. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ameelezea safari yake ya kisiasa ndani ya chama hicho huku akisema amefurahia kurudishwa kwenye kazi anayoipenda.
Aprili 4, 2024, Makalla aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo akimrithi Paul Makonda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Akizungumza na makundi mbalimbali leo Jumamosi Aprili 6, 2024 wakati akimkabidhi rasmi ofisi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Makalla ameshukuru kurudi sehemu aliyokulia akidokeza alianza kuwa mwenyekiti wa tawi kisha mwenyekiti wa kata, mwenyekiti wa Jimbo la Kawe, mhasibu mkuu wa UVCCM, katibu wa idara ya maadili na usalama wa UVCCM, naibu katibu mkuu, katibu mkuu na baadaye kuwa mweka hazina wa CCM.
“Sioni shida, naelewa na sasa nafuraha kurudi jeshini kambini nimevaa kombati. Ninayo furaha kubwa narudi kwenye kazi nayoipenda sana, naondoka katika mkoa wetu huu wa Mwanza nikiwashukuru kwa upendo mkubwa mlio onesha kwangu,” amesema Makalla.
Amesema alipoteuliwa kushika nafasi ya ukuu wa Mkoa wa Mwanza Mei 15, 2023 alianza kutumiwa ujumbe mfupi kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, kila ujumbe ukimtaka ashugulikie Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka wa fedha 2021/22 ilibaini jengo la abiria la uwanja huo lililoanza kujengwa Septemba, 2019 na kutakiwa kukamilika Mei 30, 2020, halikukamilika baada ya shuguli za ujenzi uliokadiriwa kutumia Sh13 bilioni kusimama huku vifaa vya ujenzi vya Sh233.46 milioni vilivyonunuliwa vikitelekezwa katika eneo hilo kwa zaidi ya miezi sita.
Ujenzi wa jengo hilo ulianza kutekelezwa baada ya mwishoni mwa mwaka 2018, Hayati Dk John Magufuli kuziagiza Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kushirikiana kulijenga.
Akikabidhi ofisi kwa Mtanda, Makalla amesema alipofika Mwanza, wananchi walikuwa na kiu na ndoto ya kuuona uwanja ukiwa wa kimataifa.
“Tayari kulikuwa kunajengwa jengo la abiria, lilisimamiwa na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza, lakini taarifa nilizozipata lilikuwa bado halina vigezo na lilizua maswali mengi, ukipita mtu anauliza pale ni super market?, pale ni maduka? pale kuna kitu gani? au mnaleta stendi?
“Sasa ilinipa changamoto na unajua ukiteuliwa tu tayari wewe kupitia akaunti yako ya Instagram watu wanaanza kuku-DM (kukutumia ujumbe) bwana ukifika fanya hili, kuna hili, kuna lile kwa hiyo unafika ukiwa una information (taarifa) nyingi, kwahiyo ambalo nililipata kubwa kabla hata sijafika hapa ni la Airport,” amesema Makalla.
Amesema kutokana na taarifa na kiu ya wakazi wa Mwanza, alivyofika ofisini jambo la kwanza kulishugulikia ilikuwa ni uwanja huo na kufanya uamuzi wa kuurejesha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ili isimamie.
“Kwa hiyo haikunipa shida niliporipoti tu kazi yangu ya kwanza kutoka nje ya ofisi ilikuwa kwenda pale nikakuta ofisi yangu ina jenga jengo lile kwa force account na ina Sh2.5 bilioni kwenye akaunti pamoja na kuwa chini ya ofisi ya mkuu wa mkoa, nilielewa na mimi baadaye itanitia matatizoni, nilifanya uamuzi siku ile ile kwamba ofisi yangu haina uwezo na weledi wa kujenga jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa na kuanzia leo narejesha jengo hili kwa mamlaka ya viwanja vya ndege na hela zote zilizopo katika ofisi yangu zihamishiwe huko,”amesema.
Amesema uamuzi huo ulisaidia, kwa kuwa Serikali baada ya kuona kiu ya wananchi juu ya uwanja huo ilifanya uamuzi ya kuanza ujenzi wa jengo la abiria lenye hadhi ya kimataifa ikitoa Sh28 bilioni.
“Na wiki iliyopita (Machi 28, 2024) ambayo ndio ilikuwa kazi yangu ya mwisho ya kufanya kama mkuu wa mkoa ni kusaiini mkataba; na Mungu ni mwema nilisaini mkataba wa Sh28 bilioni, unajenga jengo la abiria kwa hadhi ya kimataifa,”amesema.
Makalla amemtaka Mtanda kufanya ufuatiliaji wa ujenzi wa uwanja huo na kuhakikisha minofu ya samaki haisafirishwi kwenda Kenya na Uganda.
“Ukarabati wa kurekebisha na kuboresha jengo la mizigo unafanyika, shirika la ndege wameshakubali kuweka nafasi kwa watu watakaosafirisha mizigo ili mapato yaendelee kuongezeka badala ya sasa minofu ya samaki inasomeka inatokea Kenya,” amesema Makalla.
Vingine alivyotaja vifuatiliwe ni suala la utalii akidai Mwanza ni kitovu cha utalii na usikilizaji wa kero akiahidi kumkabidhi Mtanda kitabu chenye kero 427 alizozisikiliza.
Pia, amemtaka kufuatilia na kulisimamia tamasha la kitamaduni la Bulabo lililompa uchifu Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kuhakikisha anaisimamia timu ya mpira wa miguu ya Pamba Jiji.
Akikabidhiwa ofisi rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema ataendeleza yote yaliyoachwa na Makalla huku akiahidi kufanya ufuatiliaji maeneo yote yaliyotajwa.