Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Makalla ataja ’mifupa’ migumu Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akifungua mafunzo ya pamoja kati ya Maofisa wa Jeshi la Polisi la Mwanza, Watendaji Kata, Madiwani na viongozi wa dini jijini Mwanza yanayolenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya jamii. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Ikiwa zimepita siku 79 tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ametaja changamoto kubwa tatu alizokutana nazo mkoani humo zilizomfanya atumie nguvu kubwa kukabiliana nazo.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ametaja imani za kishirikina, vitendo vya uhalifu vikiwemo mauaji na wizi katika miradi mikubwa ya maendeleo kuwa miongoni mwa changamoto anazokabiliana nazo tangu ateuliwe kuongoza mkoa huo.

Makalla aliyeteuliwa kuongoza Mkoa wa Mwanza Mei 15, 2023 ametoa siri hiyo jana Agosti 2, 2023 alipokuwa akifungua mafunzo ya pamoja kati ya Maofisa wa Jeshi la Polisi la Mwanza, Watendaji Kata, Madiwani na viongozi wa dini jijini Mwanza unaolenga kuwajengea uwezo wa kukabiliana na kudhibiti vitendo vya uhalifu ndani ya jamii.

Mkuu huyo wa mkoa amewaambia wajumbe 280 waliohudhuria mkutano huo kuwa changamoto hizo ni miongoni mwa vikwazo vya maendeleo mkoani Mwanza.

Amesema siku za mwanzoni za uongozi wake, alikumbana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina katika Wilaya za Magu na Kwimba ambapo waganga wa kienyeji walitajwa kuwalaghai watu kuhusu utajiri kwa njia za mkato.

‘’Kwa kushirikiana na viongozi wa kijamii, Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya kazi ya kutoa elimu kwa umma kukabiliana na vitendo hivyo,’’ amesema Makalla

Akizungumzia matukio ya wizi kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Mwanza, Makalla amesema hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya wahusika zimesaidia kupunguzo vitendo vya udokozi na wizi wa vifaa katika miradi ya maendeleo.

Mafundisho na imani za kidini kupitiliza ni eneo lingine linalotajwa na RC Makalla kuwa changamoto miongoni mwa wananchi huku akitaja tukio la mtu anayejiita mchungaji wilayani Misungwi kuwakusanya wagonjwa nyumbani kwake kwa ahadi ya kuwaponya kwa maombi bila kwenda hospitali.

“Matukio yote haya tumeyadhibiti kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na wadau wengine,’’ amesema Makalla

Kamishina Msaidizi Mwandamizi (mstaafu) wa Polisi, Engelbert Kiondo aliyekuwa mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo ametaja rushwa, mmomonyoko wa maadili, mifumo mibovu ya elimu, jamii kutoshiriki vita dhidi ya uhalifu na tafsiri potofu ya imani na mafundisho ya kidini kuwa miongoni mwa mambo yanayochochea uhalifu ndani ya jamii.

‘’Jamii ni lazima isihiriki kikamilifu kudhibiti na kukabiliana na uhalifu ndipo tutafanikiwa kuwadhibiti wahalifu ambao kiuhalisia wamo ndani ya jamii,’’ amesema Kamishina Kiondo

Askari huyo mstaafu aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi katika mikoa kadhaa nchini amewahimiza viongozi wa kisiasa, kidini na kijamii kuwa kutumia ushawishi wao kusaidia vita dhidi ya vitendo vya uhalifu ndani ya jamii.

Kamishina wa Kamisheni ya Polisi Jamii Tanzania, Faustine Shilogile ametumia mafunzo hayo kuupongeza uongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano unaofanikisha kudhibiti uhalifu huku akiiomba jamii kuunga mkono juhudi hizo.