LHRC yataka uchunguzi wa haraka mauaji mtangazaji ITV

Muktasari:
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani mauaji ya mtangazaji wa televisheni ya ITV wa kipindi cha Jarida la Wanawake, Blandina Sembu na kutaka wahusika wa tukio hilo kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani mauaji ya mtangazaji wa televisheni ya ITV wa kipindi cha Jarida la Wanawake, Blandina Sembu na kutaka wahusika wa tukio hilo kukamatwa na kuchukuliwa hatua.
Mwili wa Blandina ulikutwa pembezoni mwa barabara mita chache kutoka ilipo baa ya Maryland iliyopo eneo la Mwenge, njia panda ya kuelekea ITV mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Ramadhan Kingai, mwili huo ulitupwa usiku wa Machi 27, 2021 saa 5:30 usiku kutoka katika gari aina ya Toyota Noah ambalo namba zake hazikujulikana.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 29, 2021 mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga alieleza kuwa ipo haja kwa polisi kufanya uchunguzi huo haraka ili hatua zilichukuliwe kwa wahusika.
“Tunatambua kwamba ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania 1977 inatamka bayana kwamba kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha kutoka kwa jamii yake.”
“Kinachosikitisha hatupati taarifa za kina kuhusu kifo chake maana maneno mengi yanazungumziwa kuhusu tukio hilo,” amesema Anna.
Anna amesema wanawake wenye ulemavu wamempoteza mtetezi aliyekuwa akitetea na kupambania haki zao.
“Alikuwa mtetezi mkubwa wa haki za wanawake wenye ulemavu, siku zote anaamini kile anachokifanya na siku zote wanawake wamekuwa kipaumbele chake,” amesema Henga.
Mwenyekiti wa chama cha walemavu Tanzania (Chawata), Hamad Komboza alieleza kuwa wamempoteza mwanachama na mwanaharakati hodari wa haki za watu wenye ulemavu.
Amesema Blandina alijitoa kwa moyo kuhakikisha mambo ya watu wenye ulemavu yanakwenda mbele.
“Kitendo kilichofanyika kimetuhuzunisha na kututia hofu watu wenye ulemavu, kama mwenzetu amefanyiwa mauaji ya kinyama na sisi tunapata wasiwasi. Tunaomba sheria ifuate mkondo wake wakamatwe wahusika ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema Komboza.