Polisi wafichua chanzo cha kifo cha mtangazaji ITV

Muktasari:
- Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni limethibitisha taarifa za kifo cha mtangazaji wa ITV Blandina Sembu, likieleza kuwa ni tukio la mauaji.
Jeshi la Polisi mkoa wa Kinondoni limethibitisha taarifa za kifo cha mtangazaji wa ITV Blandina Sembu, likieleza kuwa ni tukio la mauaji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Ramadhan Kingai ameeleza kuwa walipata taarifa za mwili wa Blandina kutupwa mbele ya baa ya Maryland saa tano usiku.
Amesema gari aina ya Toyota Noah ilifika katika eneo hilo na kusimama kwa muda mfupi kabla ya kutupa mwili wa Blandina akiwa tayari amefariki.
Kamanda Kingai ameeleza kuwa bodaboda waliokuwa wamepaki jirani na eneo hilo walishuhudia gari lililowashaa taa likisimama kwa dakika mbili kisha wakaona mwanamke ametupwa.
“Uchunguzi unaendelea ila tulichobaini huyu mtu hakuuliwa pale, mauaji yalifanyika sehemu nyingine pale walienda kumtupa.

“Amekutwa na majeraha usoni yanayoashiria alikuwa akijaribu kupambana kujitetea na hata jicho lake linaonekana alipigwa na kitu kizito,” amesema.
Kamanda huyo ameeleza kuwa makachero wa jeshi hilo wanaendelea na uchunguzi na muda si mrefu watawafikia waliotekeleza mauaji hayo.