‘Hausigeli’, rafiki yake mbaroni wakidaiwa kuiba kichanga

Mama mzazi wa mtoto alienusurika kutoroshwa akiwa akiwa amembeba mwanaye huyo baada ya kukabidhiwa. Picha na Hawa Kimwaga.
Muktasari:
- Kichanga kilichotoroshwa na ‘Hausigeli’ huyo kina umri wa miezi mitatu. Tayari kimerejeshwa kwa familia yake baada ya msako wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wasamaria wema.
Tabora. Mkazi wa Mtaa wa Malagarasi mkoani Tabora, mwenye umri wa miaka 15 (jina kapuni) amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kuiba na kutoroka na mtoto wa mwajiri wake, Beatrice Kiboma.
Binti huyo aliyekuwa anafanya kazi katika familia ya Beatrice yenye makazi yake Kata ya Cheyo Manispaa ya Tabora mkoani humo, anadaiwa kutoroka na kichanga hicho chenye umri wa miezi mitatu na wiki moja Machi 19, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 20, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema binti huyo amekamatwa na wananchi kwa ushirikiano na jeshi hilo, ambapo alikua akitoroka na mtoto huyo kuelekea nyumbani kwao mkoani Kigoma.
Kamanda Abwao amesema mtuhumiwa alifika Tabora Machi 18, 2025 akiwa ameongozana na rafiki yake, Coladula Deo kwa lengo la kufanya kazi za ndani na baada ya kupata kazi hiyo, aliona kazi za kufanya ni nyingi kwa mwajiri wake ndipo alipoamua kutoroka na mtoto huyo.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa kutoroka kurudi kwao na mtoto huyo kwani wakati anaondoka kwao alidanganya kuwa ana ujauzito, hivyo amelazimika kuondoka na mtoto ili akamuonyeshe nyumbani kwao,” amesema Abwao.
Abwao amesema kupitia mahojiano na binti huyo, wamebaini kuwa alikua akifanya mawasiliano na mama yake akimueleza kuwa ameshajifungua hivyo anarudi nyumbani na mtoto wake, na ndio sababu ya kutoroka na mtoto huyo.
Kamanda Abwao amesema jeshi hilo linaendelea kumshikilia ‘Hausigeli’ huyo na rafiki yake kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kauli ya familia
Beatrice ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo, amesema ‘Hausigeli’ huyo alimdanganya kuwa anaenda nje kuanika nguo za mtoto kisha kutokomea kusikojulikana.
"Alisema anaenda kuanika nguo lakini baada ya muda alitoweka na mtoto mimi nimetoka ndani baada ya kuona kengele ya kuchezea mtoto hailii tena ndio nikatoka nje kufuatilia,” amesema Beatrice.
Naye, baba mzazi wa mtoto huyo, Dotto Mwalembe amesema alipigiwa simu na mke wake kumpa taarifa ya kupotea kwa mtoto, hivyo aliwahi Kituo cha Polisi kutoa taarifa na kutokana na tayari zilikuwa zimeshasambaa zilisaidia kumpata binti huyo akiwa na mtoto wao.
“Tulimkuta akitoa fedha kwa wakala kabla ya kuingia kituo cha mabasi ili aondoke na mtoto wetu. Nawashukuru sana Polisi na jamii kwa kusaidia kumpata mtoto wetu,” amesema Mwalembe.