Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Hakuna uhusiano kati ya chafya ya mtoto na uvimbe wa titi la mama”

Muktasari:

  •  Ni mtazamo potofu ya wazazi wengi hasa wa kike kwamba inapotokea mtoto amepigia chafya titi la mama yake wakati ananyonya litauma na kuvimba


Dar es Salaam. Kama unanyonyesha na umewahi kupata uvimbe na maumivu katika titi na ukaamini chafya ya mtoto ndiyo sababu, hii inakuhusu.

Mitazamo ya baadhi ya wazazi inaeleza kuwa, maumivu ya titi wakati wa unyonyeshaji husababishwa na mtoto kupiga chafya wakati ananyonya au anapobeuwa.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wameeleza kuwa, hakuna uhusiano wowote kati ya tatizo hilo na mtoto kupiga chafya, bali ni maambukizi yanayosababishwa na mtoto kuuma chuchu.

Katika jamii, wengi wanahusisha maumivu hayo na masuala ya mila na desturi kama inavyoelezwa na Ashura Joshua, mkazi wa Iringa.

“Niliambiwa mtoto anapopigia chafya ziwa (titi) wakati ananyonya, linavimba na kuuma sana na imeshanitokea, linauma kama jipu, niliambiwa ni jambo la kimila,” amesema Ashura ambaye ni mama wa mtoto mmoja.

Kwa upande wake, Catherine Sylvester, mkazi wa Dodoma, amesema kabla ya kuwa na mtoto amekuwa akisikia kuhusu mitazamo hiyo na hata alipopata alikumbana na hali hiyo.

“Ziwa(titi) linauma hadi unapata homa. Ni maumivu ambayo wakati mwingine yanakusababisha ushindwe hata kumnyonyesha mtoto. Naepuka sana mtoto asipigie chafya ziwa (titi) wakati ananyonya,” amesema.

Mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Living Colman amesema maumivu yanayowatokea wanawake wengi yanasababishwa na vidonda vidogovidogo vinavyotokana na mtoto kuling’ata titi ili lisitoke mdomoni mwake.

Amesema mara nyingi mtoto hufanya hivyo pindi mama anaposhika vibaya titi wakati wa kunyonyesha.

“Ukweli ni kuwa mama asipomweka vizuri mtoto kwenye chuchu, mtoto anajaribu kulizuia nyonyo lisimchomoke kwa kuling’ata (hata asiye na meno), matokeo yake vinatokea vidonda vidogovidogo, kuzunguka chuchu,” amesema.

Hali hiyo ikiendelea, Dk Colman amesema wadudu waliopo mdomoni kwa mtoto (normal flora) wanaingia ndani ya chuchu na kusababisha madhara tajwa.

Kwa mujibu wa Mtaalamu huyo, madhara hayo ni maumivu na uvimbe kama jipu linalouma kupitiliza.

Amesema vidonda hivyo wakati mwingine husababisha hata chuchu kuziba na kuyafanya maziwa yashindwe kutoka, hali ambayo inaongeza maumivu zaidi.

“Ni maumivu si ya kawaida, kwani huwa ni makali sana, yanaweza kusababisha homa na mama kushindwa kuendelea kumnyonyesha mtoto,” amesema Dk Colman.

Hata hivyo, amesema maumivu hayo hudumu muda mrefu yasipopatiwa matibabu.

Kuhusu matibabu ya maumivu hayo, Dk Colman anasema ni antibayotiki maalumu na kama titi limevimba na kutengeneza jipu linapaswa kukamuliwa.

“Ili kuepuka madhara hayo inapaswa mama amuweke vizuri mtoto wake kwenye chuchu ili asimng’ate,” amesema Dk Colman.