Dar inavyobeba asilimia 86.4 ya mapato ya kodi nchini

Mwonekano wa Jiji la Dar es Salaam
Muktasari:
- Wakati mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mwaka 2022/2023 yakiongezeka kufika Sh23.658 trilioni, takwimu zinaonyesha Dar es Salaam ndiyo inaibeba maeneo mengine.
Dar es Salaam. Wakati ukusanyaji wa mapato ukiongezeka hadi kufikia Sh23.68 trilioni katika mwaka wa fedha 2022/2023 kutoka Sh21.92 trilioni mwaka uliotangulia, jambo unapaswa kujua ni kuwa asilimia 86.4 ya mapato yote yalipatikana jijini Dar es Salaam.
Ripoti ya Uchumi wa Kanda iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika mwaka huo wa fedha, inaonyesha Dar es salaam pekee ilikusanya Sh20.45 trilioni huku kiwango kinachobakia kikitoka kanda nyingine.
Takwimu hizi zisikufanye uvimbe sana mkazi wa Dar es Salaam, kwani wataalamu wanaeleza kuwa mbali na uwepo wa shughuli nyingi za kiuchumi, ubabe huo wa Dar es Salaam pia unachangiwa na kampuni kuwa na makao yake makuu katika jiji hili hata kama uzalishaji unafanya maeneo mengine ya nchi.
“Dar es Salaam inaoneka kuwa na mchango mkubwa kwa sababu ina shughuli nyingi za kiuchumi, walipakodi wakubwa kama Cocacola, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kodi ya mtu mmojammoja (wafanyakazi), kodi za forodha bandarini hivyo lazima itaonekana kuwa na kiwango kikubwa,” amesema mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude.
Pia amesema uwepo wa soko kubwa kama Kariakoo pia ni kichocheo cha kuwapo kwa mapato mengi kwa sababu linafanya kazi katika hadhi ya kimataifa.
“Hii inamaanisha kuwa, fedha nyingi inapatikana Dar es Salaam, sehemu ambayo fedha inazunguka ndiyo inaweka urahisi wa upatikanaji wake. Hali ikiendelea hivyo, Dar es Salaam inaweza kuendelea kuvutia watu wengi, mji utajaa na kufanya huduma za kijamii kuangaliwa kila mwaka,” amesema Mkude.
Amesema hali hiyo inaweza kufanya idadi ya watu kuongezeka si kwa kuzaliana bali kuhamia kutoka maeneo mbalimbali jambo linaloweza kufanya kuwapo kwa uhitaji wa maboresho ya huduma za kijamii kila mwaka.
Kanda nyingine hali ikoje?
Ripoti hiyo inaendelea kufafanua kuwa, Kanda ya Kaskazini ambayo ilikusanya Sh1.6 trilioni ndiyo inafuata baada ya Dar es Salaam ambapo makusanyo yake ni sawa na asilimia 6.8 ya mapato yote.
Kanda ya Ziwa ilifuata kwa kuchangia asilimia 2.7 katika makusanyo hayo ambayo ni sawa na Sh648.2 bilioni huku Kanda ya kati ikifuata kwa kuchangia asilimia 1.8 katika mapato hayo ikiwa ilikusanya Sh417 bilioni.
Nyanda za juu kusini ikiwa na Sh360 ambayo ni sawa na asilimia 1.5 huku Kanda ya Kusini Mashariki ikiwa na mchango wa asilimia 0.8 huku ikikusanya Sh183.5 bilioni.