Bunge latoa mwongozo mali zilizorejeshwa serikalini

Mbunge wa Manyoni Magharibi Yahya Massare, akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Utawala, Katiba na Sheria wakati wakitoa maoni yao kwenye Hotuba ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Wabunge wameshauri uwekezaji wa viwanda vya ndani na kuwawezesha wananchi katika ujuzi ili wajitegemee.
Dodoma. Bunge limeishauri Serikali kuhakikisha inafanya tathmini ya mali zote zilizorejeshwa, huku likionya kutofanya hivyo kunaweza kusababisha upotevu wa fedha kwa sababu thamani halisi ya mali hizo haijulikani.
Ushauri huo umetolewa leo Alhamisi Aprili 24, 2025 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakati ikiwasilisha maoni yake kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo, Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahya Massare amesema mali nyingi zinaweza kupotea kama hakutakuwa na taarifa sahihi kuhusu thamani yake, jambo litakalosababisha Serikali kupoteza mapato.
“Mali zinazorejeshwa serikalini lazima zithaminiwe ipasavyo, kwani bila kufanya hivyo ni vigumu kujua thamani yake halisi, hivyo kusababisha upotevu wa mapato ya Serikali,” amesema Massare.
Kamati pia, imeitaka Serikali kufanya tathmini ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na inayopangwa kutekelezwa, kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha inaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa jumla.
Aidha, kamati imependekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina ijizatiti katika usimamizi wa mashirika ya umma, kwa sababu udhaifu katika eneo hilo unasababisha kukosekana kwa gawio kwa Serikali na kupunguza mapato yake.
“Tunashauri pia Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, kuboresha vyanzo vingine vya mapato kama vile urejeshaji wa madeni yanayotokana na ubinafsishaji wa mali za umma, ili kuongeza ukusanyaji wa mapato,” amesema Massare.
Kamati pia imesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji kwa wadau wa ndani na nje ya nchi, hasa katika maeneo ya kanda maalum za kiuchumi na miradi ya kimkakati ya Taifa.
Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya amesisitiza kuwa, ili sekta ya viwanda na uwekezaji iwe na tija, Serikali inapaswa kuandaa mkakati wa kuleta wataalamu kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani.
Akipendekeza hatua za haraka, Profesa Manya ameiomba Serikali kuangazia uwezekano wa kuwaleta wataalamu kutoka India ili kuwasaidia vijana nchini kujifunza uchongaji wa vito vya madini, jambo litakaloongeza thamani ya rasilimali hizo na pato la Taifa.
“Viwanda vya ndani navyo vina umuhimu mkubwa. Tunahitaji kuviimarisha ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji, hususan gharama za umeme, hivyo kuwapa wajasiriamali faida zaidi,” amesema Manya.
Mbunge wa viti maalumu, Grace Tendega amehimiza wizara hiyo kuwekeza zaidi katika kilimo, akipendekeza jukumu hilo kukabidhiwa kwa majeshi.
Akitolea mfano eneo la Chita mkoani Morogoro linalomilikiwa na JKT, Tendega amesema eneo hilo lina rutuba, lakini halitumiki ipasavyo katika shughuli za kilimo.
“Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba. Tuweke mkazo kwenye uzalishaji kama wanavyofanya Misri. Tuwape JKT na magereza jukumu hili,” amesema.
Dk Charles Kimei, mbunge wa Vunjo amekosoa mfumo wa sasa wa uwekezaji kwa kuweka rasilimali nyingi katika maeneo machache na kuyaacha mengine nyuma, akisema jambo hilo linahitaji kupitiwa upya kwa ajili ya usawa na tija.
Ameshauri pia idara ya tathmini kupewa hadhi ya mamlaka kamili ili iweze kusimamia maeneo yanayohitaji ufuatiliaji wa karibu, akiongeza kuwa, si jambo sahihi bajeti kuongezeka kila mwaka huku uchumi ukiendelea kusuasua.
Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo ameitaka Serikali kuanzisha mchakato wa kuifuta sheria ya sasa ya kuongoza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akisema imepitwa na wakati na haiendani na mazingira ya sasa ya ukusanyaji wa mapato.