‘Akili Mnemba haikwepeki hatuna budi kuishi nayo’

Akizungumza kwenye kongamano la Akili Mnemba la Chuo cha UAUT aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Rwekaza Mukandala.
Muktasari:
- Katika kuhakikisha matumizi ya AKili Mnemba yanashiriki kwenye ukuaji wa maendeleo nchini wadau wa teknolojia, wasomi na wanafunzi wamehimiza kufundishwa kuanzia ngazi ya awali sambamba na kuitilia mkazo kisheria.
Dar es Salaam. Matumizi ya Akili Mnemba (AI) yametajwa kutokwepeka katika elimu, afya, uchumi hata uvumbuzi hivyo imepaswa kuitumia teknolojia hiyo iliyoshika kasi ili kukuza maendeleo ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
Akili Mnemba ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama vile kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi na kuwa na ubunifu katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, soko na mawasiliano.
Sambamba na hilo wadau wamehimiza umuhimu wa sera na sheria ya Akili Mnemba nchini ili kuendana na matumizi yake. Hata hivyo, Mei 10, 2025 wabunge wa Bunge la Tanzania waliibua hoja ya kuwa na sera na sheria hiyo ingawa matumizi yake yameshaanza.
Hayo yamejiri kwenye kongamano lililofanyika leo Juni 17, 2025 katika Chuo Kikuu cha United African University of Tanzania (UAUT) kilichopo Kigamboni Dar es Salaam baada ya mafunzo ya matumizi ya Akili Mnemba kwa wanafunzi na washiriki zaidi ya 150 kuanzia Juni 9 hadi 20, 2025 kwa kushirikiana na Chuo cha Mercer cha nchini Marekani.
Akizungumza kwenye kongamano hilo lenye kaulimbiu: Mustakabali wa elimu, viwanda, ubunifu barani Afrika, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Rwekaza Mukandala amesema Akili Mnemba haikwepeki lazima itumike.
“Akili Mnemba ni kama ‘Jini limeshatoka kwenye chupa huwezi kulirudisha’ kwa maana hiyo haikwepeki. Cha msingi hapa tuanze kufundisha kuanzia ngazi ya msingi ili kujengea watu uwezo zaidi,” amesema.
Profesa Mukandala amesema lazima tushiriki kwakuwa anaamini vijana wa Kitanzania wana ujuzi japokuwa wanahitaji kuwezeshwa. Lazima tuwekeze Akili Mnemba kwenye nyanja za elimu kwa wanafunzi wetu.
Profesa Thierry Nouidui, Naibu Makamu Mkuu wa UAUT, amesema lazima watu watambue ni nini Akili Mnemba inafanya vipi kazi na umuhimu wake kwa jamii.
“Tunapaswa kuwa sehemu ya ulimwengu wa Akili Mnemba, kutumia, kufundisha wanafunzi ili waitambue. Natamani walimu wa msingi wafundishe ili iwe rahisi wanafunzi kuitambua. Teknolojia hii ni rasilimali lazima itumike,” amesema.
Loicy Mkeu, mkazi wa Dar es Salaam aliyeshiriki mafunzo hayo amesema Akili Mnemba inasaidia na kadiri miaka inavyokwenda na teknolojia hiyo inakua hivyo watu wanapaswa kujifunza licha ya vitisho kuwa ni hatari.
Mwanafunzi wa chuo hicho, Collin Mujjuzi, akitolea mfano sehemu ambazo mwanadamu hawezi kufikia kama kufanya tafiti akili mnemba inaweza kutumika ikiwa kama fursa.
Vivian Ngashweki, mwanafunzi wa chuo hicho amesema mafunzo aliyoyapata yamemsaidia kusoma na kutatua changamoto zake za kielimu kupitia Akili Mnemba.
Naye Godlisten Stanley, mwanafunzi wa mwaka wanne chuoni hapo aliyebuni mfumo wa utambuzi wa chuma au uvimbe kwenye teknolojia ya MRI Scan amesema mafunzo hayo yamemsaidia kuboresha zaidi kwenye mfumo huo.
“Akili Mnemba inasaidia mfumo huu wa utambuzi kwa hiyo inaweza kutumika kwenye hospitali na kuokoa maisha pamoja na sekta ya afya kwa ujumla,” amesema Stanley.
Naye Dennis Mwighusa, Mkurugenzi Mtendaji taasisi ya Utafiti ya Akili Mnemba barani Afrika (Arifa) amesisitiza umuhimu wa elimu kwa umma na sera madhubuti kuhusu Akili Mnemba.
"Hakuna haja ya kuogopa kuongezeka kwa Akili Mnemba. Ni zana muhimu katika zama hizi za mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia. Lakini ili kupunguza hofu ya umma, lazima tuweke mifumo imara ikiwemo sera, mikakati, na miongozo ili kukuza matumizi yake yenye uwajibikaji," amesema.