Aga Khan inavyoshiriki utekelezaji Malengo Endelevu ya Maendeleo

Muktasari:
- Mradi wa Choice unatoa mwanga wa kuwekeza kwa wanawake na wasichana ili kuharakisha utekelezaji wa SDG kupitia usawa wa kijinsia, afya ya akili na mazingira.
Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam (AKHD) imedhamiria kuharakisha kufikia Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG) namba 3, 5, na 13 kupitia ushirikiano wa pamoja, uhamasishaji, na miradi ya ubunifu.
Malengo hayo yanalenga afya bora na ustawi, usawa wa kijinsia, na hatua za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kutekeleza dhamira hiyo, kwa kushirikiana na mradi wa Choice kutoka Taasisi ya Afya ya Kimataifa na Maendeleo, Chuo Kikuu cha Aga Khan Pakistan, leo Machi 27, 2024 imewakutanisha wataalamu wa afya na wadau wa kijinsia jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2024 kwa kujadili malengo hayo kupitia kaulimbiu isemeyo "Wekeza katika jinsia ya wanawake: Kuharakisha maendeleo."
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.
Mradi wa Choice unatoa mwanga wa kuwekeza kwa wanawake na wasichana ili kuharakisha utekelezaji wa SDG kupitia usawa wa kijinsia, afya ya akili na mazingira.
Akizungumzia mradi huo unaotekelezwa katika nchi tano za Tanzania, Kyrgyzstan, Ghana, Kenya na Pakistan, Daktari Bingwa wa Mionzi kutoka Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, Profesa Ahmed Jusabani amesema nchi nyingi hazijafikia malengo hayo kutokana na athari zikiwemo za Uviko 19.
Amesema mradi huo unalenga kuwatumia wanazuoni waliopo katika nchi husika kuangalia Taifa limefikia wapi katika utekelezaji wa malengo hayo, kutambua changamoto na kutafuta suluhisho kuwezesha utekelezaji wa SDG ifikapo mwaka 2030.
“Mradi huu utakuwa na matokeo nchi nzima kwa sababu tutaongeza uelewa kwa watu, tutafundisha kuanzia kada za chini waelewe athari hata katika afya ya akili,” amesema Profesa Jusabani.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Huduma za Afya za Aga Khan Tanzania, Sisawo Konteh amesema hatima ya Taifa inategemea kuwekeza katika maendeleo ya wanawake na wasichana na ustawi wao, utakaoleta maboresho katika sekta zote, hivyo utekelezaji wa mradi huo una tija kubwa.
Mratibu wa Kitaifa wa Muungano wa Tanzania wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi (GCCTC), Maria Matui amesema wamegundua mabadiliko ya tabianchi yanazidi kutambulika na kuongezeka kwenye jamii, hivyo kunapaswa kuongeza wigo kuwagusa moja kwa moja wanajamii ambao kimsingi ndiyo waathirika.
“Tunafahamu mfano joto linaongezeka, hivyo athari zipo hadi kwenye kilimo na maji jambo ambalo linaleta athari katika mfumo wa afya ya akili, na nyingi zinazoathiri maisha yetu ya kila siku,” amesema na kuongeza:
“Hivyo mpango uliopo sasa tunaangazia namna gani wanajamii watahusika moja kwa moja katika kutoa mapendekezo na ushauri ili kutoa maamuzi juu ya mabadiliko na athari zake.”
Amesema jitihada zinapaswa kuendelea katika kumkomboa mwanamke ambaye ndiye mwathiriwa mkuu wa athari hizo, akitoa mfano wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Matui amesema kuna mikakati mbalimbali ya kitaifa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi na inayohusu afya ya akili ambayo inafahamika na wachache, kwa kuwa bado haijawafikia wananchi wa kawaida.
“Hivyo, Aga Khan wameona hiyo changamoto na wao wakiwa kama watoa huduma ndani ya nchi wametoa fursa hii kwa kuongeza mfumo wa afya ili kuwafikia wadau wengi zaidi, wapate ufahamu juu athari zote zinazotokana na mabadiliko hayo yanavyoathiri afya na jinsia,” amesema.