Aga Khan kuwanoa vijana wajasiriamali

Mkurugenzi Mkaazi wa Mfuko wa Aga Khan, Abdi Mallick akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu mdahalo maalumu wa vijana utakaofanyika kesho kujadili namna bora za kujikita katika biashara. Picha na Ericky Boniphace
Muktasari:
- Kutumia mdahalo kujifunza kwa wenzao waliofanikiwa
- Mdahalo huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kesho, pamoja na mambo mengine utajadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo vijana hususan kwenye suala la kujiajiri.
Mfuko wa Aga Khan kwa kushirikiana na asasi za kiraia umeandaa mdahalo utakaowakutanisha zaidi ya vijana 250, kujadili namna bora ya kujikita kwenye biashara.
Mdahalo huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kesho, pamoja na mambo mengine utajadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo vijana hususan kwenye suala la kujiajiri.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Aga Khan, Abid Mallick alisema ajira limekuwa tatizo kwa vijana hivyo wameangalia namna ya kuwasaidia kukabiliana nalo.
Mallick alisema vijana wengi wamekuwa wanahitimu elimu ya juu na kukosa kitu cha kufanya licha ya kuwa na utaalamu mbalimbali, jambo linalosababisha kufanya vitu bila kuwa na uhakika na matokeo yake.
Alieleza kupitia mdahalo huo, vijana watapata nafasi ya kujifunza, kujieleza na hatimaye kufanya uamuzi sahihi katika ujasiriamali.
Mkurugenzi huyo alisema mwaka 2016, Taasisi ya Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ilifanya utafiti kuhusu mitazamo, matamanio na malengo ya vijana kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda na kwamba, matokeo yalionyesha ukosefu wa ajira ni kitu pekee kinachowaathiri vijana.
Mkakati wazinduliwa
Katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana, Mfuko wa Aga Khan umezindua mradi wa kilimo biashara (Agro-Business) ili kuongeza kipato kwa wakulima 5,000 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kupitia mpango unaotambulika kama Scale Program, mawakala hao wameandaa majadiliano na ushirikiano ili kuunga mkono jitihada za vijana wajasiriamali.
Kuhusu utafiti uliofanyika, Mkurugenzi wa Taasisi ya Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan, Alex Awizi alisema kulingana na utafiti uliofanywa mwaka 2014, asilimia 58 ya vijana nchini wangependa kuanzisha biashara zao lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Badala ya kuwaacha waingie mtaani na kujiingiza katika biashara ambazo zitawaacha maskini, tuwasaidie, ” alisema Awizi.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Ekihya, Lillian Sechelela alisema mdahalo huo utawawezesha vijana kujifunza kwa wengine ambao wamefanikiwa.
Sechelela alisema wajasiriamali vijana licha ya kuzungumza na kuwaeleza wenzao uzoefu katika biashara, watapata nafasi ya kuonyesha bidhaa zao.
“Nafasi kama hizi huwaongezea vijana uwezo wa kupanua biashara zao na kufikiri vitu vikubwa, badala ya kuwaza kuajiriwa,” alisema Sechelela.