37 wabainika kuugua kipindupindu Kanda ya Ziwa, mmoja afariki dunia

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Pima Sebastian (mwenye suti nyeusi) akizungumza wakati wa kikao cha dharura cha kamati ya afya kilichozungumzia kupambana, kutokomeza na kuzuia kusambaa kwa kipindupindu jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.
Muktasari:
- Mikoa ya Mwanza na Shinyanga yaguswa zaidi, idadi ya wagonjwa yaongezeka kutoka watano hadi 18.
Mwanza/Shinyanga. Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 37 wanaendelea na matibabu ya ugonjwa wa kipindupindu ulioibuka katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.
Kwa mara ya kwanza mlipuko wa ugonjwa huo uliripotiwa Januari 6, 2024 ambapo watu watano waliugua kipindupindu katika eneo la mji mdogo wa Kagongwa mkoani Shinyanga.
Taarifa iliyotolewa leo Januari 9, 2024 kutoka mkoani Shinyanga imesema wagonjwa wameongezeka na kufikia 18 kati ya hao, Manispaa ya Kahama ina wagonjwa 15, Manispaa ya Shinyanga mmoja na ya Kishapu wawili.
Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumanne Januari 9, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Rachel Kasanda amesema aliyefariki dunia ni mwanamume aliyekuwa ametoka kwenye sherehe iliyofanyika kwa mmoja wa wake zake anayeishi Dutwa, mkoani Simiyu.
Kasanda amesema mwanamume huyo baada ya kutoka Dutwa alirejea kwa mwanamke mwingine anayeishi wilayani Magu akiwa na dalili za kuharisha na kutapika.
Amesema hali yake ilipobadilika alipelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Magu ambako alifariki dunia akiwa mapokezi.
"Baada ya kupata taarifa ndugu wa marehemu wanaoishi Dutwa walikuja msibani Magu, lakini tulizuia matanga na kuwatawanya lakini wachache waliobaki nao walikuwa wameshapata ugonjwa hivyo tukawapeleka zahanati ya Bugatu iliyopo Magu ambayo tumeifanya kituo cha kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu na wanaendelea na matibabu," amesema Kasanda.
Kuhusu Nyamagana na Ilemela, Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dk Pima Sebastian amesema watu saba wamethibitika kuugua kipindupindu, 18 wakiwamo ndugu na waliokutana nao wanafanyiwa ufuatiliaji.
"Watu wawili walibainika Januari 4, 2024 eneo la Kakebe, Igoma jijini Mwanza, wakasema wametokea Simiyu. Baada ya kuwabaini tuliwapeleka kituo cha uangalizi kilichopo Mkuyuni jijini Mwanza,” amesema.
Dk Pima amesema baadaye ugonjwa huo uliripotiwa eneo la Mkolani na katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela.
Amesema wagonjwa wawili wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya matibabu ambao afya zao zimeimarika.
Dk Pima amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
"Ugonjwa huu unaambukiza kwa kula hovyo chakula, maji au kitu chochote chenye vimelea vya kipindupindu. Tunahamasisha jamii kunawa mikono wakati wote wakitoka kujisaidia au kabla ya kula," amesema.
Pia ameonya watu wanaokula chakula kilichopoa akisema kina uwezekano mkubwa wa kuhifadhi vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.
Amependekeza kuwapo uratibu wa uuzaji chakula mtaani ili kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala ameagiza watumishi wa jiji hilo kufanya kazi hadi siku za mapumziko (Jumamosi na Jumapili) hadi pale mkakati wa kudhibiti ugonjwa huo usisambae utakapopatikana.
"Naagiza magari ya matangazo (PA) yapite kila mahali kutoa taarifa ya uwepo wa ugonjwa huo na namna ya kujikinga. Pia tuwe na mpango wa kuhakikisha ugonjwa huu hausambai katika taasisi zikiwamo shule za msingi, sekondari na kwenye magereza," amesema Salala alipozungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.
Naye ofisa usafi na mazingira Mkoa wa Mwanza, Desderius Polle ametangaza kuanza msako wa watu wanaonunua chakula kwa mamalishe wanaotoa huduma hiyo katika maeneo yasiyo rasmi.
"Tunaanza msako kuwakamata wanaonunua chakula kwa mamalishe waliopo maeneo ambayo si rasmi kwani wanaweza kuchangia kusambaza ugonjwa huu. Tutawakamata kwa sababu ndiyo wanasababisha wauze chakula hicho," amesema Polle.
Hali Shinyanga
Mkoani Shinyanga imeripotiwa idadi ya wagonjwa imeongezeka kutoka watano hadi kufikia 18.
Mkuu wa mkoa huo, Christina Mndeme akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Januari 9, 2024 amefafanua kuwa vifo vitano vilivyotokea katika Kata ya Kagongwa vilisababishwa na kuhara na kutapika.
Amesema baada ya vifo hivyo kutokea, timu ya wataalamu ilifika katika kata hiyo kuchunguza chanzo cha ugonjwa wa kuhara na kutapika.
Mndeme amesema baadhi ya wananchi waliohudhuria mazishi ya familia zilizopoteza ndugu ni miongoni mwa waliothibitika kuugua kipindupindu wakiwamo ndugu.
Amesema kati ya wagonjwa 41 waliolazwa kwenye vituo vilivyotengwa kati yao 18 wamethibitika kuwa na kipindupindu na wamepatiwa matibabu.
Mndeme amesema hakuna kifo kilichothibitika kutokea kutokana na ugonjwa huo.
"Vifo vitano vilivyotokea ambavyo wanne walifia katika jamii na mmoja kituo cha afya wakati akipatiwa matibabu havikuthibitika kama wamekufa kwa kipindupindu kwa kuwa hawakupimwa," amesema.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafi na kuwa na matumizi sahihi ya vyoo.
Pia amehimiza usafi wa mazingira ili kujiepusha na maradhi yakiwemo magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake, mratibu wa ufuatiliaji na udhibiti magonjwa ya kuambukiza Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu, amesema tayari wamechukuwa hatua ya kutoa elimu kwa jamii, wakiwamo mama na babalishe na maeneo ya mikusanyiko.
Amesema kutokana na mlipuko wa kipindupindu, wamepiga marufuku uuzaji wa vyakula maeneo ya shule ili kulinda afya za watoto na walimu.
Pia wamezuia vyakula kuuzwa maeneo yote ya vilabu vya pombe ili kuzuia ugonjwa kusambaa.