Chunya wajihadhari magonjwa ya milipuko

Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya, Saimon Mayeka Saimon
Muktasari:
- Mkuu wa Wilaya ya Chunya ametoa siku saba kwa wananchi kufanya usafi kwenye makazi na maeneo ya biashara, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa kwa watakaokaidi.
Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka ameagiza viongozi wa ngazi za kata na vijiji kutumia sheria ndogo za halmashauri kuwabana wananchi wanaojihusisha na tabia za uchafuzi wa mazingira, kwa lengo la kukabiliana na mlipuko wa magonjwa.
Sambamba na hilo, Mayeka ametoa siku saba kuhakikisha wananchi wote wanazingatia maagizo hayo na watakaokiuka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ili kulinda afya za wananchi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Novemba 28, 2023 ikiwa ni siku tatu tangu afanye mkutano wa hadhara wa wananchi katika kijiji cha Ifumbo wilayani humo kutatua mgogoro wa ardhi na kuhamasisha suala la usafi wa mazingira amesema. “Nasisiza suala la usafi zingatieni, viongozi tumieni sheria ndogo za halmashauri kwani zipo wazi kwa watu wanaokiuka msisubiri kusukumwa au mpaka kuibuka kwa magonjwa ya milipuko” amesema Mayeka.
Ameongeza kuwa “Kwa sasa tunaelekea kwenye msimu wa mvua nyingi kutaibuka magonjwa ya kipindupindu, mnatambua hivi karibuni tumetoka kupambana na ugonjwa wa kichocho ili tusifike huko suala la usafi lizingatiwe ”amesema.
Wakati huohuo, Mkuu huyo wa Wilaya, amesisitiza jamii hususani wakulima kuzingatia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kupanda kwa wakati ili kuepuka madhara kufuatia uwepo wa mvua nyingi katika msimu huu.
“Ndugu zangu wanachunya chukueni taadhari ya mvua nyingi ili kuepuka majanga yanayoweza kujitokeza sambamba na suala zima la usafi,” amesema.
Kwa upande wake ,Diwani Kata ya Ifumbo,Weston Mpyila amesema watatekeleza agizo hilo huku akishukuru Serikali kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi ya elimu, afya maji na miundombinu ya barabara.
“Tunahitaji Sh77 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo cha afya, tunaomba mkuu wa wilaya tusemee jambo, kwani umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” amesema.
Mkazi wa Chunya, Alex Naftari amesema suala la usafi lizingatiwe kwani kuna changamoto za baadhi ya wananchi wamekuwa akifungulia uchafu pindi mvua inaponyesha, hali ambayo inaweza kusababisha magonjwa ya milipuko.