Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zelensky adai Putin anamuogopa, ataja sababu

Rais wa Ukraine, Voloymyr Zelensky

Muktasari:

  • Tangu itangaze operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, Russia imeyatwaa maeneo ya mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk, Zaporizhia na Crimea iliyotwaliwa na Russia kutoka Ukraine tangu mwaka 2014.

Kyiv. Rais, Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema yupo tayari kuonana na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Rais, Vladimir Putin wa Russia.

Zelensky ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 14, 2025, huku akimkejeli Rais Putin kuwa anaogopa kuonana naye hususan kwenye mkutano uliopangwa kufanyika Alhamisi wiki hii.

Hata hivyo, Russia bado haijathibitisha iwapo Rais Putin atashiriki katika mazungumzo yaliyopangwa kufanyika kesho (Alhamisi) Istanbul nchini Uturuki.

Endapo watakutana itakuwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa mzozo huo hatari zaidi barani Ulaya miaka mitatu iliyopita, unatajwa pia kuwa hatari zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia (WWII).

Mazungumzo hayo yanatajwa kuwa kitovu cha juhudi za amani zinazoongozwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye mbali na kuonyesha nia ya kuhudhuria amesema atamtuma Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.

Trump pia amesema viongozi wengine wa Marekani watakaohudhuria ni wajumbe waandamizi, Steve Witkoff na Keith Kellogg,

Zelensky amesema anataka kujadiliana juu ya usitishaji mapigano wa siku 30 usio na masharti kama hatua ya kuelekea kumaliza vita na Putin anapaswa kushiriki kwa sababu kila kitu nchini Russia kinamtegemea yeye.

“Tunataka kukubaliana juu ya mwanzo wa mwisho wa vita. Yeye (Putin) anaogopa mazungumzo ya moja kwa moja nami,” amesema Zelensky.

Zelensky amesema anatarajia Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) zitaiwekea vikwazo vikali Russia iwapo mazungumzo hayatafanyika.

Alipoulizwa ni nani atawakilisha Russia kwenye mazungumzo hayo, Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisema: “Mara tu rais atakapopenda, tutatangaza.”

Katika hatua nyingine, mashambulizi yaliyotekelezwa na Russia usiku wa kuamkia leo yameua takriban watu watatu katika mkoa wa Kharkiv nchini Ukraine.


Trump kuhudhuria?

Wakati wa hotuba yake nchini Saudi Arabia, Trump alisema Rubio ndiye atahudhuria mazungumzo hayo ya Alhamisi, pamoja na wengine.

“Tutaona kama tunaweza kufanikisha hili,” alisema Trump jana. Hata hivyo, Kellogg, katika mahojiano ya awali na Fox Business Network, alisema Trump atajiunga na mazungumzo hayo Istanbul iwapo Putin atahudhuria.

“Tuna tumaini Rais Putin pia atafika kisha Rais Trump atakuwa hapo. Hili linaweza kuwa tukio la ajabu sana. Amani inaweza kupatikana, naamini kwa kweli, haraka sana iwapo viongozi hao watatu wataketi pamoja na kuzungumza,” alisema Kellogg.

Kellogg aliieleza Televisheni ya Fox kuwa Ukraine ipo tayari kukubali usitishaji mapigano ambapo vikosi vya Ukraine na Russia vitajiondoa kila upande kwa kilomita 15, na kuunda eneo lisilo na silaha (Demilitarized zote (DMZ).


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.