Zaidi ya 297 wafariki Gaza ndani ya saa 24

Muktasari:
- Israel imeendeleza mapigano yake dhidi ya wanamgambo wa Hamas, huku Wapalestina zaidi ya 297 wakiripotiwa kufariki dunia kutokana na mapigano hayo ndani ya saa 24.
Gaza. Mapigano makali yamesababisha vifo vya takribani Wapalestina 297 ndani ya saa 24 zilizopita huko Gaza, huku kundi la Hamas na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakirushiana vitisho.
Mashambulizi ya Israel yaliendelea katika eneo lililozingirwa jana Jumapili, ikiwa ni pamoja na Kaskazini mwa Gaza ambako vitongoji vyote vimeathiriwa na mashambulizi ya anga.
Katika eneo hilo, askari wa ardhini wa Israel wamekuwa wakifanya kazi kwa zaidi ya wiki sita, licha ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa wapiganaji wa Hamas.
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Gaza, Ashraf al-Qudra aliiambia Al Jazeera katika mahojiano ya simu kuwa watu 297 waliuawa na zaidi ya 550 kujeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita huko Gaza.
Idadi ya vifo tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas huko Gaza, imezidi kuongezeka hadi kufikia zaidi ya 18,000.
Mapigano hayo ambayo yalizuka Oktoba 7 mwaka huu, yamesababisha takribani vifo 18,000 kwa Wapalestina, huku upande wa Israel ikiwa ni zaidi ya 1,000.
Idadi ya majeruhi imeendelea kukua hadi 49,229 kwa Palestina na Israel 8,730.
Israel iliendeleza mapigano makali mapema wiki iliyopita, baada ya muda wa makubaliano wa kusitisha mapigano, ili kupisha misaada ya kibinadamu kuingia Gaza kumalizika.
Hata hivyo, inaaminika kuwa huenda mapigano hayo yakasitishwa wiki chache zijazo kabla ya Sikukuu ya Krismasi au mwishoni mwa mwaka, huku Marekani ikionyesha kuwa na wasiwasi juu ya idadi ya vifo.