Israel yakubali kuongeza muda zaidi kusitisha vita

Muktasari:

  • Israel imekubali kuongeza muda wa kusitisha vita kwa muda ili kuruhusu mateka zaidi wanaoshikiliwa na Wanamgambo wa Hamas kuachiliwa, huku ikielezwa kuwa haya yanafanyika baada ya Rais wa nchi hiyo, Isaac Herzog kukutana na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kwamba mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas wanaachiwa.

Dar es Salaam. Kufuatia mazungumzo ya upatanishi yanayoendelea ili kumaliza vita baina ya Israel na Hamas, muda wa kusitisha mapigano unatarajiwa kuongezwa baada ya Israel kuridhia huku ikipokea orodha mpya ya mateka watakaoachiwa huru.

DW imeripoti kuwa taarifa ya Israel kukubali muda huo kuongezwa, zimetolewa na Qatar ambaye ndiye mpatinishi huku ikisema na kwamba makubaliano hayo yanaendana na masharti ya awali.

Taarifa hii ya kuongezwa muda huo inajiri wakati ambapo Jeshi la Israel (IDF), limesema mateka wengine sita zaidi wamekabidhiwa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu na kwamba wako njiani kuelekea Israel.

Hii inapelekea idadi jumla ya mateka wa Israeli walioachiwa hapo jana, kufikia watu nane.

Imeelezwa kuwa mapema siku hiyo ya Alhamisi, Hamas waliwakabidhi maofisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu, mateka wengine wawili wa kike.

Kwa mujibu wa DW, haya yote yanafanyika baada ya Rais wa Israel Isaac Herzog kukutana na mwenzake wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, kandoni mwa mkutano mazingira (COP28), kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kwamba mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas wanaachiwa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Herzog imesema kwamba Rais huyo wa Israel ametoa wito kwa Rais Al Nahyan, kutumia kikamilifu ushawishi wake kisiasa, kuhakikisha kwamba mateka wa Israel wanaachiliwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amewaambia waandishi wa habari mjini Tel Aviv kwamba, amemweleza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kwamba nchi hiyo inapaswa kuweka mikakati ya kuwalinda raia kabla kuanza tena operesheni yake kusini mwa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani amesema Israel, ni mojawapo ya jeshi lenye nguvu zaidi duniani ambalo lina uwezo wa kutuliza kitisho cha Hamas na wakati huo huo kupunguza hasara kwa watu wasio na hatia. 

Blinken ameongeza kuwa Israel imekubaliana kuhusiana na suala hilo la kuwalinda raia.

Kwa upande mwingine, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), anatarajiwa kufanya ziara nchini Israel, kufuatia ombi la waathirika wa shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Mahakama ya ICC imeongeza kuwa Khan anatarajiwa pia kuizuru Ramallah katika Ukingo wa Magharibi, kukutana na maafisa wakuu wa Palestina.

Katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter, ICC imesema ziara hiyo si kwa ajili ya kufanya uchunguzi ila ni ziara inayotoa fursa ya kutoa pole kwa wahanga na kufanya mazungumzo nao.

Hata hivyo, Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa IDF imesema kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, Wanamgambo wa Hamas walifyatua risasi dhidi ya Israel, na hivyo kukiuka masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Awali Israel ilisema ilizuia roketi iliyorushwa kutoka Gaza huku vyombo vya habari vinavyoshirikiana na kundi la Hamas vikiripoti milipuko na milio ya risasi kaskazini mwa Gaza.

Makubaliano ya kusitisha mapigano hayo yalipangwa kudumu kwa siku nne lakini muda uliongezwa mara mbili.

Hadi kufikia Alhamisi, mateka 110 waliokuwa wameshikiliwa huko Gaza wameachiwa huru tangu kuanza kwa mapatano hayo tarehe 24 Novemba, huku Israel ikiwa imewaachia huru wafungwa 240 wa Kipalestina.

Mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba yaliua watu 1,200.

Tangu wakati huo, Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema zaidi ya watu 14,800 wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel, wakiwemo watoto wapatao 6,000.