Israel, Hamas wajadili kuongeza muda mabadilishano ya mateka

Israel/Gaza. Kwa nyakati tofauti pande zote mbili za Israel na Hamas zinajadili mpango wa kuongeza siku za kubadilishana mateka wa vita yao iliyodumu kwa miongo kadhaa.
Hayo yanajiri ikiwa ni siku ya mwisho ya zoezi hilo lilofanyika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ili mateka wa vita hiyo hasa wanawake na watoto warudi katika maeneo yao ya asili.
CNN imeripoti kuwa Hamas ina mpango kurefusha mapatano yake ya siku nne na Israel.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili jioni Novemba 26, 2023, Hamas ilisema inataka "kuongeza muda wa kusitisha mapigano baada ya muda wa siku nne kumalizika, kupitia juhudi kubwa za kuongeza idadi ya wale walioachiliwa kutoka jela kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano ya kibinadamu."imesema sehemu ya taarifa ya Hamas.
Mapema wikendi hii, Qatar, ambayo ilichukua jukumu kuu katika upatanishi wa makubaliano hayo, ilisema pia ilikuwa na matumaini ya kuongeza muda wa usitishaji vita, ambao unajumuisha utoaji wa kuongeza siku moja ya ziada kwa kila mateka kumi ambao Hamas iko tayari kuwaachia.
Hayo yalisemwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed Al-Ansari, aliiambia CNN Jumamosi.
Pia, Baraza la Mawaziri la Vita la Israeli lilijadili uwezekano wa kuongeza makubaliano ya muda wa mabadilishano wa mateka na Hamas wakati lilipokutana Jumapili jioni, chanzo cha Israeli kiliiambia CNN.
Chanzo hicho kilisema masharti ya kuongezwa muda bado hayajabadilika kutoka kwa makubaliano ya awali, ambayo ina maana kwamba Hamas inatakiwa kuwaachilia mateka wengine 10 kwa kila siku ya ziada ya kusitisha mapigano.
Israel na Hamas walifikia makubaliano wiki iliyopita kwa kusitisha mapigano kwa siku nne na mpaka jana jioni waliachiliwa takribani wanawake 50 na watoto waliokuwa mateka huko Gaza.
Rais wa Marekani ,Joe Biden pia alionyesha kutaka kuongezwa muda wa kusitisha mapigano wakati wa hotuba yake Jumapili.