Waandamanaji Kenya wavamia na kupora mali za wabunge

Muktasari:
- Maandamano ya vijana Kenya yaliyoanza wiki mbili zilizopita, yakilenga kupinga vifungu vya muswada wa fedha
Eldoret. Waandamanaji katika Mji wa Eldoret wamevamia klabu moja inayohusishwa na mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi anayedaiwa kuwa mshirika wa Rais wa Kenya, William Ruto.
Umati wa watu waliokuwa wamevaa fulana nyeusi na viakisi mwanga walivamia klabu ya Timba XO na kuharibu mali na kupora pombe zilizokuwemo.
Klabu hiyo iliishia kuwa uwanja wa vita kati ya polisi na waandamanaji hao walioanzisha makabiliano makali na wasimamizi wa sheria.
Kwa jumla, kulikuwa na fujo leo Jumanne Juni 25, 2024 huku milio ya risasi za mabomu ya machozi, moshi, mioto mikubwa, nyimbo na kelele vikitawala muda wote.
Maduka yalikuwa yamefungwa huku wafanyabiashara wakijiweka mbali na mji na baadhi ya wakazi wakijiunga na maandamano mapema siku hiyo, huku wengine wakisimama kutazama.
Waandamanaji hao wamesema hawajafurahishwa na Serikali ya Kenya wakiishutumu kutojali Wakenya.
Katika Mji wa Nyeri, vijana waliwazidi nguvu polisi na kuingia Supermarket ya Chieni inayohusishwa na Mbunge wa Kieni, Njoroge Wainaina.