Mtu mmoja auawa uvamizi wa Bunge Kenya, wengine wapigwa risasi

Waandamanaji Kenya wakiwa nje ya majengo ya Bunge jijini Nairobi leo Juni 25, 202. Picha na NMG
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti ya Daily Nation, polisi walifyatua risasi na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa
Nairobi. Bunge la Kenya leo Jumanne Juni 25, 2024 limezingirwa na waandamanaji wanaopinga ongezeko la kodi ambao waliingia bungeni.
Vijana hao walifanikiwa kulifikia jingo la Bunge baada ya kuwazidi nguvu polisi waliokuwa wakidhibiti maandamano hayo, jambo lililowasukuma kuanza kutumia nguvu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Daily Nation, polisi walifyatua risasi na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.
“Polisi wamewapiga risasi waandamanaji wanne na kumuua mmoja, kama ilivyoshuhudiwa na KHRC (Tume ya Haki za Binadamu cha Kenya). Tunalaani vikali mauaji ya polisi. Vitendo kama hivyo havikubaliki na ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Haki na uwajibikaji ni muhimu. Tutasukuma kwa nguvu zote uwajibikaji wa polisi,” inaeleza KHRC ikituma ujumbe kwenye mtandao wa X baada ya mapigano hayo.
Kabla ya kuingia bungeni, ripoti zinaonyesha kuwa waandamanaji wasiopungua 10 walipigwa risasi na kujeruhiwa.
Muda mfupi baada ya kupigwa risasi, sehemu ya jingo la Bunge ilichomwa moto, hivyo kuzua taharuki.
Wabunge waliokuwa wakiendelea na shughuli zao, walitoroka kupitia njia za chini kwa chini huku waandamanaji wa kupinga kodi, wakivamia mgahawa na kutishia kuingia kwenye chumba cha mijadala.
Polisi wameonekana wakitumia risasi za moto katika kujaribu kuwazuia vijana kuingia kwenye jengo hilo huku waandamanaji wengine wakikaribia kutoka City Hall Way na Uhuru Highway.
Picha za video kutoka maeneo ambayo wabunge hujadili masuala ya kitaifa na kutunga sheria zinaonyesha kuwa sehemu ya Seneti ilikuwa inawaka moto huku mabomu ya machozi yakisambaa kila kona ya eneo hilo.
Makabiliano hayo mabaya ya leo yalikuwa kilele cha azma ya maandamano ya “kulidhibiti Bunge” huku waandamanaji wengi wao wakiwa vijana wakisimama kidete kuhakikisha muswada huo unatupiliwa mbali.
Saa chache kabla ya tukio hilo la ajabu la ujasiri ambao haujawahi kuonekana awali, maelfu ya vijana waliandamana kwenye barabara na mitaa kadhaa ya Nairobi huku biashara zikifungwa tangu asubuhi.
Hadi kufikia leo saa nne asubuhi, polisi na vijana walikuwa wakicheza mchezo wao wa paka na panya huku maofisa waliovaa sare wakiwarushia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha wakiwalenga waandamanaji hao.
Hata hivyo, habari zilipoenea kwamba Bunge lilikuwa limepitisha muswada huo, waandamanaji zaidi na zaidi walimiminika mjini.
Machafuko haya yametokea wakati vijana katika kaunti zisizopungua 30 walipoingia mitaani kupinga muswada wa fedha.
Machafuko ya Nairobi yalizua upya kumbukumbu za mwaka 2014 huko Burkina Faso.
Katika mwaka huo, waandamanaji wenye hasira waliingia bungeni katika Mji Mkuu wa Ouagadougou na kuchoma moto baada ya upinzani wao mkubwa dhidi ya mipango iliyotaka kumruhusu Rais Blaise Compaore kuongeza muda wa utawala wake wa miaka 27.