Prime
Vituko vya mbwa wa marais, mmoja afukuzwa Ikulu

Rais wa Russia, Vladimir Putin akiwa kwenye mazungumzo na aliyekuwa Cansela wa Ujerumani, Angel Makel huku mbwa wa Putin akiwa mbele yao. Picha na mtandao
Wakati mbwa wa Rais Joe Biden wa Marekani akiondolewa Ikulu kwa kujeruhi walinzi 11 wa kiongozi huyo, nchini Ufaransa mbwa wa Rais Emanuel Macron wamesababisha hasara kwa kutafuna samani, kuzirarua na kuvunja vitu vya thamani.
Nchini Russia, mbwa mkubwa mweusi wa Rais Vladimir Putin aitwaye Konni alitumika kujenga hofu na hasa kwa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel anayeogopa wanyama hao.
Mbwa wa Rais Biden
Nchini Marekani mbwa wa Rais Biden aitwaye ‘kamanda’ aina ya German Shepherd amewajeruhi walinzi 11 wa kiongozi huyo kwa siku tofauti.
Taarifa ya kituo cha televisheni cha CNN cha Marekani kuhusu mbwa kamanda anavyojeruhi walinzi Ikulu ya White House na kwenye makazi ya familia yaliyopo Delaware, ndiyo ilimuibua Elizabeth Alexander, msemaji wa Jill Biden, mke wa Rais Biden aliyekiri mbwa huyo kujeruhi walinzi 11 na kwamba ameondolewa Ikulu.
"Rais na mkewe wanajali usalama wa wale wanaofanya kazi katika Ikulu ya White House na wale wanaowalinda kila siku," ni kauli ya Elizabeth Alexander kwa vyombo vya habari.
Elizabeth alisema familia ya Rais Biden inawashukuru walinzi kwa subira na kwamba mbwa huyo ameondolewa White House.
Taarifa ya CNN kuhusu mbwa huyo ilisema idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya iliyotajwa, ikielezwa majeruhi mmoja alipelekwa hospitali kwa matibabu zaidi na wengine walitibiwa eneo la tukio.
Maofisa wa Ikulu walieleza juhudi zao za kutoa mafunzo kwa mbwa huyo ili asijeruhi watu, lakini haikuwezekana.
Rekodi za matukio ya mbwa huyo kujeruhi zinaeleza Oktoba 26, 2022 alimjeruhi mlinzi baada ya mke wa Rais, Jill Biden kushindwa kumdhibiti.
Baada ya tukio hilo, ofisa mwingine wa usalama aliandika baruapepe akilalamika ameng’atwa mara mbili na mbwa huyo, huku mwingine aliyeshuhudia tukio akisema walilazimika kutumia mkokoteni wa chuma kujikinga ili ashiwashambulie.
Kwa mujibu wa taarifa, matukio hayo yaliripotiwa kwa mkurugenzi wa usalama, Kimberly Cheatle. Desemba 11, 2022 mbwa kamanda alimshambulia mlinzi mbele ya Rais Biden kwenye mkono na kidole gumba.
Mbwa huyo alipelekwa Ikulu mwaka 2021, ikiwa ni zawadi kwa Rais Biden iliyotolewa na kaka yake, James.

Rais wa Ufaransa, Emanuel Macron akitembea katika Ikulu ya Elysee Palace akiwa na mbwa wake, Nemo. Picha na mtandao.
Hasara Ufaransa
Mbwa wa Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy akiwa madarakani kuanzia Mei 16, 2007 hadi Mei 15, 2012, walisababisha hasara kwa kutafuna samani, mazulia na hata Ikulu yake kuitwa jina la utani la ‘nyumba ya mbwa’
Rais Sarkozy alipokuwa madarakani alikuwa na mbwa wengi waliopewa majina ya Toumi, the chihuahua, Clara, Dumbledor na the labradors, ambao walidaiwa kutafuna samani na mazulia yaliyohifadhiwa kwenye chumba cha kumbukumbu ya vitu vya kihistoria ndani ya Ikulu.
Vituko vya mbwa wa Sarkozy vilitawala kwenye magazeti kutokana na taarifa kuwa walitafuna samani kwenye chumba ambacho Napoleon alitia saini mwaka 1815.
Pia, mbwa hao wanadaiwa kuharibu vitu vya thamani, milango na kukojoa kwenye masofa.
Taarifa za jarida la Mediapart, zinaeleza uharibifu huo hasa wa vitu vilivyotengenezwa kwa nakshi ya majani, matengenezo yake yaligharimu fedha nyingi.
Sarkozy, aliyezaliwa Januari 28, 1955 alitawala Ufaransa kwa muhula mmoja akiwa Rais wa 23 na baadaye alifungwa jela kwa tuhuma za rushwa.
Tuhuma dhidi ya utovu wa nidhamu wa mbwa wa Sarkozy zinaeleza wanyama hao waliharibu vyombo vya thamani ndani ya Ikulu kwa kuvunja kioo cha vito vya mapambo vyenye umri wa zaidi ya miaka 200.
Vyanzo vya habari ndani ya ofisi inayosimamia mali za kale 70,000, zilidai mbwa hao pia waliharibu milango na baadhi ya vitu.
Mke wa Sarkozy, Bruni-Sarkozy alipohojiwa na jarida ya Femmes Actuelles mwaka 2009 kuhusu utovu wa nidhamu wa mbwa wake, alisema wa kwanza, wa pili na wa tatu walikuwa na tabia nzuri na chanzo cha furaha, lakini walipoongezeka hali ilibadilika.

Rais wa Marekani, Joe Biden akiwa na mbwa wake. Picha na mtandao
Mbwa Konni wa Putin
Rais Valmidir Putin wa Russia, ambaye anaelezwa kupenda wanyama ana mbwa mkubwa mweusi aitwaye Konni.
Mara kadhaa inaelezwa alikuwa akimtumia kumtia hofu Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alipokuwa madarakani.
Kwenye mkutano wao wa Januari 2007 katika mji wa Sochi nchini Russia, Rais Putin anadaiwa kumtumia Konni kumtia hofu Markel kwa kuruhusu awepo ndani ya chumba cha mkutano akirandaranda, ikiwamo kumnusa Merkel.
Inaelezwa Rais Putin alitambua kuwa Merkel anaogopa mbwa, hivyo kwenye vikao vyao Putin alikuwa anakwenda na mnyama huyo, hali iliyomfanya Kansela Merkel kutokuwa na utulivu kwenye mazungumzo.
Merkel alizaliwa Julai 17, 1954 na ni mwanafizikia na mwanasiasa aliyekuwa Kansela wa Ujerumani tangu Novemba 22, 2005 hadi Desemba 8, 2021.
Vyombo vya habari vya magharibi kuna wakati viliandika kuhusu diplomasia ya Russia na Ujerumani kwamba inaonekana Merkel anaogopa mbwa na Putin anafahamu ukweli huo.
“Kwa hivyo, wakati wowote Putin anapokutana na Merkel huko Moscow, anahakikisha mbwa wake naye anakuwa kwenye chumba cha mazungumzo.”
Taarifa ya msaidizi wake ilisema woga wa Merkel dhidi ya mbwa unatokana na kung'atwa na mnyama huyo alipokuwa mdogo na tangu wakati huo amejiweka mbali nao.
Kuna wakati mbwa wa Putin aliingia kwenye chumba cha mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na Merkel ambaye ghafla alitamka kwa lugha ya Kirusi; "Sasa mbwa atakula waandishi wa habari."
Hata hivyo, mwandishi wa habari Yulia Latynina aliyekuwa akiandikia gazeti la Yezhednevny zhurnal aliandika kuwa, Putin alimwambia Merkel:
"Sidhani kama mbwa atakutisha. Hatafanya chochote kibaya, anapenda waandishi wa habari.”
Latynina alisema katika mkutano wa kirafiki uliofanyika mjini Sochi, kuingia kwa mbwa Konni kwenye chumba cha mazungumzo kulimwacha Merkel akiwa amechanganyikiwa.
“Mbwa alipomkaribia na kumnusa, Merkel aliganda, akionekana kuwa na hofu. Alikuwa ameumwa mara moja, mwaka 1995; hofu yake ya mbwa hakuweza kumkimbia Putin,” alisema.
Kwa mujibu wa mwandishi huyo, Merkel alitafsiri tabia ya Putin. “Ninaelewa kwa nini anapaswa kufanya hivi - ili kuthibitisha kuwa yeye ni mwanamume," aliwaeleza waandishi wa habari na kuongeza:
"Anaogopa udhaifu wake mwenyewe. Russia haina chochote, haina siasa yenye mafanikio au uchumi. Walicho nacho ni hiki tu.”
Russia imekuwa ikitumia wanyama kuwapinga viongozi wengine duniani. Mfano, Putin aliwahi kumwambia Rais wa Marekani George W. Bush kuwa: "Mbwa wangu ni mkubwa kuliko wako."
Hata hivyo, Rais Putin aliwahi kunukuliwa na gazeti la Ujerumani la Bild akisema kitendo chake cha kuwa na mbwa wakati wa mazungumzo yake na Merkel hakuwa na lengo la kumtisha.
"Nilitaka kumfanyia kitu kizuri. Nilipogundua hapendi mbwa, bila shaka niliomba msamaha," aliliambia gazeti hilo.
Imeandaliwa na Noor Shija, kwa msaada wa mtandao.