1, 000 wanaougua kichaa cha mbwa, wawili hupona

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Mpwapwa wakiwa wamejitokeza ili kuwapatia mbwa wao chanjo kwenye maadhimisho ya kichaa cha mbwa yaliyofanyika Kitaifa Wilayani humo.
Muktasari:
- Leo ni maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa Duniani ambapo imeelezwa kati ya watu 1,000 wanaougua ugonjwa huo ni wawili au mmoja ndiyo wanaweza kupona.
Mpwapwa. Imeelezwa kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni hatari kwa binadamu kwani kati ya watu 1,000 wanaopata ugonjwa huo ni mmoja au wawili ndiyo wanaopona.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Septemba 28, 2023 na Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk Rogath Kishimba kwenye maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa yaliyofanyika Kitaifa Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Dk Kishimba amesema gharama za kutibu ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni kubwa kuliko chanjo inayotolewa hivyo ili kukabiliana na tatizo hilo ni wajibu wa wananchi wanaofuga mbwa kuwapa chanjo kwa wakati na kuwafungia ndani ili wasizurure ovyo mitaani.
Amesema chanjo ya kichaa cha mbwa na paka zinapatikana kila mahali nchini kwa gharama ndogo, hivyo wafugaji wa wanayama hao wahakikishe wanawapa chanjo kwa wakati ili wasisababishe madhara kwa wafugaji na jamii inayowazunguka.
"Gharama ya chanjo ni ndogo sana unaweza kulipia Sh500 au Sh1, 000 kwa mwaka lakini gharama ya kumtibu mtu aliyepatwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni kubwa kwani hupelekea kifo ambayo ndiyo gharama kubwa kuliko pesa zitakazotumika kumtibia," amesema Dk Kishimba.
Amesema chanjo ya kuzuia ugonjwa huo kwa mtu aliyeng'atwa na mbwa inagharimu kati ya Sh25, 000 hadi Sh75, 000 kulingana na hospitali atakayofika kupata huduma huku dozi yake ikiwa ni kati ya tatu hadi tano.
Amesema kuzuia ugonjwa huo kwa mbwa na paka ni rahisi kuliko kuzuia ugonjwa huo kwa mtu aliyeng'atwa na mnyama mwenye virus vya kichaa cha mbwa kwani madhara yake ni makubwa kuliko kwa wanyama.
Dk Kishimba amesema virusi vya kichaa cha mbwa humuathiri mtu aliyeng'atwa kuanzia kwenye jeraha hadi kwenye mfumo wa fahamu ambapo huchukua kati ya siku 20 hadi 90 kuanza kuonyesha dalili za ugonjwa kutegemeana na eneo alilong'atwa
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Gerald George amesema Wizara hiyo imekuwa ikitoa elimu ya kuchanja mifugo yao ili kujikinga na ugonjwa huo kwani unaathiri zaidi watoto ambao ni Taifa la kesho.
Amesema waathirika wakubwa wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni watoto kwani wana tabia ya kucheza na mbwa wanaozurura mitaani bila kujua kama wana kichaa hivyo wao ndiyo kundi lililo kwenye hatari zaidi.
Naye Ofisa Tarafa wa Mima, Irene Milinga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, amesema Wilaya hiyo imepokea chanjo za kutosha kwa ajili ya kuchanja mbwa ambazo zitaendelea kutolewa muda wote ili wananchi waendelee kuchanja na kujiepusha na ugonjwa huo hatari.