Vijana wa Gen-Z Kenya, waanzisha chama chao cha siasa

Muktasari:
- Vijana wa Kenya, maarufu Gen-Z wameanzisha chama chao cha siasa walichokipa jina la ’47 Voices of Kenya Congress’ ambacho tayari kimeingia kwenye uwanja wa siasa baada ya kusajiliwa rasmi.
Kenya. Vijana wa Kenya, maarufu Gen-Z wameanzisha chama chao cha siasa walichokipa jina la ’47 Voices of Kenya Congress’ ambacho tayari kimeingia kwenye uwanja wa siasa baada ya kusajiliwa rasmi.
Kupitia chama hicho vijana hao ambao katika miaka ya hivi karibuni wamegonga vichwa vya habari nchini humo ikiwemo kwenye maandamano wamedhamiria kuwakilisha sauti za jamii na makabila 47 ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa DW.
Hata hivyo, kulingana na sensa ya 2019 zaidi ya asilimia 75 ya Wakenya 47.6 milioni wana umri chini ya miaka 35 na katika usajili wa wapiga kura mwaka 2022, kulikuwa na wapiga kura 8,811,691 wa kati ya umri wa miaka 18 na 34 wakiwa asilimia 40 ya wapiga kura wote huku idadi hiyo ikikadiriwa kuongezeka zaidi ifikapo 2027.
Katika uchaguzi uliopita, zaidi ya nusu ya Gen-Z walikuwa chini ya umri wa kupiga kura. Zaidi ya vijana milioni 14 wa Gen Z watahitimu kupiga kura mwaka wa 2027 ikiwa ni ongezeko la asilimia 79.4 ya kundi hilo.
Wakenya wa umri wa miaka 18 hadi 34 watakuwa milioni 17.8 na kuwa katika nafasi muhimu ya kuamua mwelekeo wa siasa za Kenya kutoka mwaka 2027. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Taifa Leo.
Kupitia kauli mbiu yake ‘sauti kila mahali’ chama hicho kipya cha kisiasa nchini Kenya, kinachoongozwa na vijana kimedhamiria kuangazia masuala na matarajio ya vijana nchini.
Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Wycliffe Kamanda amesema chama chenyewe kimejengwa kwenye misingi ya ubunifu, uadilifu na ushirikishwaji wa kila Mkenya bila kuzingatia asili au eneo anakotoka.
Chama hicho kimepata usajili rasmi kutoka kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na sasa, wako kwenye kampeni ya kitaifa wakiwahimiza vijana kujiandikisha kama wapiga kura.
Vijana wa Gen-Z kwa miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakipinga Serikali ya Rais William Ruto, tangu kupinga ongezeko la ushuru na hali mbaya ya kiuchumi kwa vijana wa Kenya pamoja na kupinga Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024.
Katika mwaka huo 2024 maandamano yalifanyika huku vijana 60 wakiuawa na vikosi vya usalama katika wiki za maandamano ya kupinga hatua hizo za Serikali.
Kufuatia hilo Gen-Z walipanga kufanya maandamano ya maadhimisho Juni 25, 2025 ambayo awali yalikuwa ya amani ingawa muda ulivyozidi kwenda vurugu zikaibuka ndipo hekaheka ilipoanza ikiwemo mabomu kurindima huku watu 16 wakiuawa.
Aidha, tofauti na maandamano ya Juni 25, 2025 ya kumbukizi ya vifo vya watu 60 waliouawa mwaka jana 2024 kwenye maandamano mengine yalifanyika ya kutafuta haki kwa mwanahabari, Albert Ojwang aliyefariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi jijini humo.