Kenya yazuia maandamano ya Gen-Z kuoneshwa mubashara

Muktasari:
- Uamuzi wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja umepingwa na vituo vya NTV, KTN na Citizen TV, pamoja na Jukwaa la Wahariri, wakisema ni uvunjaji wa sheria na kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Nairobi. Maandamano yanayoendeshwa na kizazi cha Gen-Z Kenya yamefanya Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kuagiza vituo vyote vya televisheni na redio kuacha kurusha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano hayo yanayoendelea.
Uamuzi huo umelalamikiwa na vituo vikubwa binafsi vya televisheni, ikiwamo NTV na KTN, ambavyo vimesema polisi walivamia vituo vyao na kuzima matangazo, huku Kituo cha Citizen TV kikiripoti kuwa polisi walifika, lakini hawakuzima matangazo.
Aidha, Jukwaa la Wahariri Kenya nalo limepinga uamuzi huo wa kuzuia matangazo ya moja kwa moja, likisema unakiuka sheria pamoja na uhuru wa vyombo vya habari.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano, David Mugonyi, inaeleza kuhusu hatua kali zitakazochukuliwa dhidi ya vyombo vya habari vitakavyokiuka agizo hilo.
Kupitia barua rasmi, mamlaka hiyo imezielekeza televisheni na redio zote nchini kusitisha mara moja matangazo ya moja kwa moja ya maandamano, ikionya kwamba kutotii agizo hilo kutasababisha kuchukuliwa kwa hatua za kisheria.
Vituo vya televisheni vya NTV, KTN
Hata hivyo, vituo binafsi vya televisheni vya NTV na KTN vimeripoti kuwa baada ya kutolewa kwa tangazo hilo, polisi pamoja na maofisa wa mawasiliano waliingia katika vituo vyao na kuzima matangazo.
“Kufungiwa kwa NTV ni kuingilia moja kwa moja shughuli zetu za uhariri,” inaeleza kampuni mama ya NTV, Nation Media Group, katika taarifa yao.
Kituo kingine binafsi, Citizen TV, kimeripoti kuwa maofisa hao walifika katika kituo chao cha matangazo wakiwa na nia ya kuzima matangazo yao.
Hata hivyo, matangazo ya vituo hivyo yanaendelea kwenye YouTube na mitandao ya kijamii.
Maandamano yameenea katika sehemu mbalimbali za nchi huku polisi wakizidi kupelekwa kudhibiti hali hiyo.
Uamuzi huo pia, umelalamikiwa na Kampuni ya The Standard Group ikisema itatafuta njia za kisheria kuthibitisha uhalali wa agizo hilo.
The Standard Group kwenye taarifa yake imeeleza msimamo wake kuhusu vyombo vya habari kuzuiwa kurusha moja kwa moja maandamano hayo.
“Wakati tunaendelea kurusha matangazo kwa masilahi ya umma, msimamo wetu ni kwamba agizo hili ni kinyume cha sheria na linakiuka moja kwa moja sehemu za 33 na 34 za Katiba na sheria mama ya nchi.
“Zaidi ya hayo, Sheria ya Habari na Mawasiliano ya Kenya ya 1998 (KICA) haisemi kuwa CA ina mamlaka au idhini ya kuchukua hatua kama ilivyotishia.
“Kwa hivyo, tutamshitaki mtu yeyote anayefunga vituo vyetu vya matangazo bila maelezo yoyote yanayokubalika kisheria, kwa haki na kwa busara. Tunatarajia masharti ya mikataba yatekelezwe kikamilifu; ukiukaji wowote utaibua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na fidia kwa hasara zitakazojitokeza.
“Tunaomba CA iachie tishio hilo na itekeleze jukumu lake la udhibiti kwa mujibu wa sheria za nchi na haki ya kimsingi,” inaeleza taarifa ya The Standard Group.
Jukwaa la Wahariri
Rais wa Jukwaa la Wahariri nchini Kenya, Zubeida Kananu amekosoa agizo hilo na pia kutishia kuishtaki mamlaka hiyo kwenye Mamlaka ya Bodi ya Vyombo vya Habari ya Kenya (MCK), ambayo ina mamlaka ya kushughulikia malalamiko dhidi ya vyombo vya habari.
“Ninachosoma hapa ni kuingilia kati. Wanajaribu kudhibiti vyombo vya habari. Wamefanya hivi, si mara moja tu, bali mara nyingi kabla. Kwa nini hawawezi kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi yao ya kuwajulisha Wakenya kuhusu kinachoendelea?,”amehoji Kananu.
Chama cha Waandishi wa Habari
Chama cha Waandishi wa Habari Kenya kimeshutumu agizo la Serikali la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya kwenye televisheni na redio.
Chama hicho kimesema matangazo ya moja kwa moja si tishio bali ni kazi ya kiraia ya kuhakikisha uwajibikaji na uwazi.
“Tunahimiza vyombo vya habari vyote kusimama kidete na kuheshimu uamuzi wa mahakama kuu wa mwaka 2023 uliozuia ukandamizaji huo,” inaeleza taarifa ya chama hicho.