Prime
Simulizi waliotekwa na Hamas siku 471

Muktasari:
- Mmoja ya mateka hao amedai alifanyiwa upasuaji bila ganzi wakati akiishi chini ya ardhi.
Gaza. Romi Gonen (24), Emily Damari (28) na Doron Steinbrecher (31) wamesimulia namna walivyoishi chini ya ardhi kwa zaidi ya miezi 15 baada ya kutekwa nyara na wapiganaji wa Hamas wa Palestina.
Waisrael 251 walitekwa katika shambulizi lililoua zaidi ya watu 1,200 Oktoba 7, 2023 baada ya Hamas kuvamia Israel katika sherehe iliyokuwa ikifanyika Kusini mwa taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Baada ya uvamizi huo Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi katika Ukanda wa Gaza ulioua Wapalestina zaidi ya Gaza zaidi ya 46,899 huku 110,725 kujeruhiwa hadi mapigano yalipofikia hatua ya makubaliano ya usitishwaji wiki iliyopita, huku mateka na wafungwa wakiachiwa.

Wakifanya mahojiano na vituo vya habari ya Israel na kuchapishwa katika tovuti ya The Times of Israel pamoja na BBC, Waisrael hao waliokabidhiwa Januari 19 kwa maofisa wa kikosi cha Msalaba Mwekundu wamesimulia walichokipitia walivyokuwa chini ya ardhi.
Wamesema waliogopa kifo katika hali ambayo hawakuona mwanga kwa siku 471. Gonen alitekwa nyara kwenye maandamano ya Supernova karibu na Kibbutz Re’im Oktoba 7, 2023 huku Damari na Steinbrecher walitekwa kutoka kwenye nyumba zao karibu na Kibbutz Kfar Aza.
“Sikufikiria kama ningeweza kurudi. Nilidhani ningefia Gaza," mmoja wao amenukuliwa na Channel 12.
Mwingine amedai alifanyiwa upasuaji bila ganzi wakati akiwa chini ya ardhi.
Damari na Gonen wamesema walipigwa risasi wakati wa shambulio. Damari alipoteza vidole viwili kutokana na jeraha lake.
Damari, raia wa Uingereza na Israel amesema kuachiliwa huru kwake ni kama ‘amefufuka’.
Pia, katika chapisho la Instagram kutokana na kuachiliwa kwake, Damari pia ameandika "I love, I love, I love" (napenda, napenda, napenda), namshukuru Mungu, familia ya na marafiki wa karibu zaidi nilionao katika ulimwengu huu."
Ingawa walikuwa chini ya ardhi wamesema mara kwa mara walikuwa wakionyeshwa habari za televisheni na redio, ikiwa ni pamoja na maandamano ya kuitaka serikali kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka hao.
Watatu hao walikuwa mateka wa kwanza kuachiliwa katika hatua ya awali ya mapatano hayo ya awamu tatu, ambayo yanatoa kwa jumla ya mateka 33 kuachiliwa kwa muda wa siku 42 pamoja na wafungwa wa Kipalestina.
Familia zatoa shukrani
Jana Jumatatu, wazazi na ndugu wa mateka hao watatu walioachiwa walifanya mkutano na waandishi wa habari katika Kituo cha Matibabu cha Sheba na kusema wote walikuwa wanaendelea vizuri kiafya.
Pia walitoa shukrani kwa serikali, wapatanishi, Rais wa Marekani Donald Trump, na watu wa Israel kwa usaidizi wao na usaidizi katika kuwarudisha wapendwa wao nyumbani.
Inaaminika mateka 91 kati ya 251 waliotekwa nyara na Hamas wamesalia Gaza, ikiwa ni pamoja na miili ya takriban 34 iliyothibitishwa kuuawa na Jeshi la Israel (IDF).
Mateka wanne wamepangwa kuachiliwa Jumamosi ijayo. Kwa muda wa wiki nne zifuatazo, mateka watatu wataachiliwa kila Jumamosi, hadi kundi la mwisho la 14 katika siku ya 42 ya kusitisha mapigano.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wafungwa wa Kipalestina ambao ni wanawake na watoto waliokamatwa na Jeshi la Israel (IDF) na kufungwa katika magereza nchini humo wameachiwa usiku wa kuamkia jana Jumatatu Januari 20, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusitishwa kwa vita kati ya IDF na Hamas.
Hata hivyo, idadi kamili ya Wapalestina ambao wanashikiliwa na kuwekwa vizuizini nchini Israel tangu kuanza kwa mapigano hayo Oktoba 7, 2023, bado haijafahamika hadi sasa.