Safari ya saluni ilivyokatisha uhai wa mwanafunzi Chuo Kikuu

Ann Karambu, Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Kiriri ambaye inasaidikiwa kuwa alibakwa kabla ya kukutwa na umauti yake

Kenya. Familia moja katika Kijiji cha Kabuboni, Kaunti ya Tharaka-Nithi, inapambana kutafuta haki ya binti yao mwenye umri wa miaka 21, aliyeuawa kikatili.

Mwili wa Ann Kambura ulikutwa umetupwa kisimani huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma wakati blauzi na sidiria yake vikiwa vimefungwa kwa nguvu shingoni kwake na hivyo kuashiria kuwa aliuawa kwa kunyongwa.

Ann ambaye alikuwa mwanafuzi mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Kiriri, aliondoka nyumbani Ijumaa Mei 12, mwaka huu saa 8.30 mchana kuelekea saluni kusuka ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kurudi chuoni jijini Nairobi siku iliyofuata, hata hivyo hakurejea tena.

James Mwiti, baba wa Ann na mkewe Frida Gaceri wameuambia mtandao wa ‘Nation’ kuwa walimpigia simu binti yao muda wa saa 7 usiku kujua kama alikuwa amehudumiwa kwa sababu muda ulikuwa umeenda, hata hivyo; simu hiyo hakupokea.

Wazazi waliendelea kupiga simu lakini hakupokea na baada ya saa chache simu ilizima huku wakidhani binti yao aliamua kulala nyumbani kwa msusi wake baada ya kuona giza limeingia.

Kesho yake asubuhi, walimpigia tena simu ambayo ilikuwa bado imezimwa, kitu kilichosababisha wahisi huenda kuna kitu kibaya kimetemtokea na hivyo kuamua kwenda huko saluni kupata taarifa kamili.

Hata hivyo, Msusi aliwaeleza kuwa Ann alifika kwenye saluni hiyo saa tatu usiku na kuondoka mwendo wa saa 06:30 baada ya kumaliza kusuka nywele zake.

Kwa kuwa wazazi hao walikuwa na wasiwasi juu ya binti yao, waliamua kumtafuta mwendesha bodaboda aliyempeleka saluni, ambay alithibitisha kwamba Ann alikuwa amefika saluni, lakini hakuwa amempigia simu kumrudisha nyumbani.

Baada ya majibu hayo, wazazi waliamua kupigia simu marafiki wa Ann chuoni ili kujilidhisha ikiwa binti yao aliamua kurudi chuoni, hata hivyo marafiki hao kwa nyakati tofauti walisema chumba chake kilikuwa kimefungwa, kitu ambacho kiliashiria kuwa alikuwa hajarudi chuoni.

"Ijumaa hiyo, nilitumia siku nzima kufuatilia mkopo niliokuwa nimeomba kwaajili ya kumlipia ada yake, japo ndiyo siku aliyouawa,” alisema Gaceri.

Wazazi hao waliripoti suala hilo kwa chifu wa eneo husika na matangazo yakatolewa katika makanisa ya eneo hilo, huku msako ukianza.

Siku ya Jumatano, rafiki wa familia hiyo, Jeremy Thirika, aliwashauri pia kuripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Chuka, lakini walipofika huko, walishauriwa kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi karibu na makazi yao.

Wakati wanaandikisha taarifa za tukio hilo kituoni hapo, taarifa za kipolisi kutoka kwa afisa wake mmoja, zilikitaarifu kituo hicho juu ya kupatikana kwa mwili uliokuwa umetupwa katika kisima kimoja kijijini hapo.

Gaceri alisema kwamba kutokana na maelezo ya saizi na mavazi, alikuwa na uhakika kwamba taarifa hiyo ilimhusu binti yake.

Kwa pamoja na Polisi, walielekea eneo la tukio na, baada ya kuopoa maiti, familia ilithibitisha kwamba alikuwa Ann.

Mwili huo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Chuka huku Polisi wakianza uchunguzi kuhusu tukio hilo.

“Binti yangu ameuawa kikatili kwa sababu kisima kilifunikwa vizuri, mikono na kichwa chake vilikuwa vimefungwa kwa blauzi yake iliyochanika na ilikuwa imefungwa kwa nguvu shingoni,” baba wa marehemu alisema kwa hisia kali.

Mwiti ameambia ‘Nation’ kuwa ripoti ya uchunguzi wa maiti ilionyesha Ann ambaye ni mtoto wake wa kwanza, alibakwa kabla ya kuuawa.

Baba huyo alijiapiza kutomzika binti yake hadi pale watu waliofanya uhalifu huo watakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.

Hata hivyo, mpaka tunaenda mitamboni, polisi walikuwa hawajamkamata mshukiwa yeyote kuhusiana na kitendo hicho cha kinyama, huku wazazi wakiendelea kuomba haki kutendeka kwa binti yao ambaye walikuwa na matarajio makubwa juu yake.

Katika taarifa yake, Gavana wa Kaunti hiyo, Muthomi Njuki ameelezea wasiwasi wake kutokana na visa vya uvunjaji sheria katika kaunti yake.

"Nimesikitishwa sana kwamba msichana wa miaka 21, Ann Kambura Mwiti, ambaye alikuwa akijiandaa kurejea chuo, alibakwa na kuuawa kikatili katika eneo letu tena mtaani kwake," Njuki amesema katika taarifa hoyo, na kuongeza;

"Hii haikubaliki kabisa na inatishia amani na utulivu ambao tumekuwa tukifurahia. Haiwezi kuwa kwamba kama viongozi wa kaunti hii, tunaketi chini na kutazama hali hii ya sasa inayoendelea.”

Gavana huyo amesisitiza kuwa familia ya Ann inastahili haki na kutoa wito kwa vyombo vya uchunguzi kuharakisha kesi na hivyo kuhakikisha kuwa wote waliohusika wahusika wanafikishwa mahakamani.