Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Leo XIV afuata nyayo za watangulizi wake

Muktasari:

  • Papa Leo wa XIV alizaliwa Septemba 14, 1955 mjini Chicago, Illinois, Marekani ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu, alichaguliwa katika wadhifa huo Mei 8, mwaka huu.

Vatican. Papa Leo XIV amechapisha ujumbe wake wa kwanza kwenye akaunti rasmi za mitandao ya kijamii za Papa, ambazo awali zilitumiwa na watangulizi wake, Papa Francis na Papa Benedict XVI.

Papa Leo XIV ameamua kuendeleza mwenendo wa watangulizi hao kwenye mitandao wa X na Instagram.

Idara ya Mawasiliano ya Vatican imethibitisha Papa kuandika machapisho hayo leo Jumatano Mei 14, 2025.

Ujumbe wa Papa kwenye Instagram umetokana na hotuba yake ya kwanza kwa umma aliyoitoa muda mfupi baada ya kuchaguliwa Mei 8, 2025, ulioambatanishwa na picha kadhaa kutoka siku za kwanza za upapa wake.


Amani iwe nanyi nyote! Hili ndiyo salamu ya kwanza aliyotoa Kristo Mchungaji Mwema aliyefufuka. Napenda salamu hii ya amani ipenye ndani ya mioyo yenu, ndani ya familia zenu, na miongoni mwa watu wote, popote walipo, katika kila taifa na kote ulimwenguni,” ameandika Papa Leo.

Katika taarifa hiyo, Idara ya Mawasiliano Vatican imeeleza kuwa akaunti rasmi ya @Pontifex kwenye X ina jumla ya wafuasi milioni 52 ikichapisha maudhui katika lugha tisa.

Maudhui yaliyokuwa yakichapishwa na mtangulizi wake, Papa Francis yatahifadhiwa katika sehemu maalumu ya tovuti rasmi ya Vatican (www.vatican.va).

Kwenye Instagram, akaunti mpya ya Papa itakuwa na jina @Pontifex – Pope Leo XIV, ambayo ndiyo itakuwa akaunti pekee rasmi ya Kipapa kwenye jukwaa hilo, linalomilikiwa na kampuni ya Meta.

Taarifa kutoka Vatican zinasema kuwa akaunti ya Papa Francis, @Franciscus, itaendelea kupatikana kama kumbukumbu ya kihistoria.

Papa Francis alidumisha utamaduni wa kuwepo kwenye majukwaa hayo mawili ya mitandao ya kijamii, akichapisha takribani machapisho 50,000, mengi yakiwa ni vifungu vya hotuba zake kwenye mtandao wa X na picha kutoka matukio yake ya umma kwenye Instagram.

Kwa mujibu wa Vatican, machapisho hayo ya kila siku karibu kipindi chote cha upapa wa Papa Francis, yalibeba ujumbe mfupi wa kiinjili na maudhui kuhusu amani, haki ya kijamii, na utunzaji wa mazingira.

Mwaka wa 2020 pekee, maudhui ya mitandao ya kijamii ya Papa Francis yaliangaliwa zaidi ya mara bilioni 27.


Papa Benedict mwongoza njia

Papa Benedict XVI ndiye alikuwa Papa wa kwanza kufungua akaunti ya mitandao ya kijamii, alipoweka chapisho la kwanza ‘tweet’ ya Kipapa akiwa na umri wa miaka 84, kwenye mtandao wa Twitter, Desemba 12, 2012.

“Marafiki wapendwa, ninafuraha kuwasiliana nanyi kupitia Twitter. Asanteni kwa mwitikio wenu wa ukarimu. Nawabariki nyote kutoka moyoni mwangu,” aliandika Papa huyo mzaliwa wa Ujerumani.

Ujumbe wake uliokuwa na herufi 140 ,ulifungua mlango kwa Vatican kuukumbatia mfumo wa mawasiliano wa kisasa hususan ni mitandao ya kijamii.

Baada ya kuchaguliwa kuwa Papa wa 266, Papa Francis alitumia akaunti hiyohiyo ya Twitter, na ujumbe wake wa kwanza ulikuwa:

“Marafiki wapendwa, nawapongeza kutoka moyoni na nawaomba muendelee kuniombea.”

Machi 19, 2016, Papa Francis alipanua uwepo wa Kipapa kwenye mitandao kwa kufungua akaunti yake ya Instagram, @franciscus. Chapisho lake la kwanza lilikuwa ni picha yake akiwa amepiga magoti akiomba, ikiwa na maneno: “Niombeeni” kwa lugha mbalimbali.

Papa Leo XIV anapoitumia mitandao ya kisasa ya mawasiliano, taasisi za kanisa, Wakatoliki na wasio Wakatoliki wanaweza kuangalia uongozi wake na kupata msukumo wa namna ya kujihusisha na mitandao kwa hekima na maadili.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira wa msaada wa mashirika ya habari.