Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Francis kuzikwa Jumamosi Vatican

Muktasari:

  • Mwili wa Baba Mtakatifu Francis unatarajiwa kuwekwa kwa heshima kuanzia kesho Jumatano katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican

Vatican. Mazishi ya Papa Francis yanatarajiwa kufanyika Jumamosi Aprili 26, 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali, Giovanni Battista Re, ambaye ni Dekano wa Baraza la Makardinali.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Vatican leo Jumanne Aprili 22, 2025, mwili wa hayati Papa Francis utawekwa ndani ya Kanisa hilo kuu kuanzia kesho ili kutoa fursa kwa waamini na watu wote kutoa heshima zao za mwisho, kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani.

​Papa Francis alifariki dunia Jumatatu Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88, kutokana na ugonjwa wa kiharusi. Kifo chake kilitokea katika makazi yake ya Domus Sanctae Marthae, Vatican.

Kiongozi huyo wa kiroho amefariki akiwa na maono ya mwisho yaliyojikita katika kuhimiza amani na udugu wa kibinadamu, akisema kuwa mateso aliyoyapata katika siku za mwisho wa maisha yake ameyatoa kwa Bwana kwa ajili ya amani ya dunia na mshikamano miongoni mwa wanadamu.


Sababu za kifo chake

Taarifa iliyotolewa na Vatican inaeleza kuwa kabla ya kufariki Papa Francis (88) aliugua ugonjwa wa kiharusi hali iliyosababisha moyo kushindwa kufanya kazi, huku ikidokeza kuwa madaktari walifanya jitihada kurudisha moyo katika hali ya kawaida lakini ilishindikana.

"Papa amefariki kutokana na kiharusi,” inaeleza sehemu ya taarifa rasmi ya sababu ya kifo cha Papa Francis iliyochapishwa katika tovuti rasmi wa Vatican.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Papa Francis.

Hati ya kifo cha kiongozi huyo wa kiroho imetaja magonjwa mengine yaliyokuwa yanamsumbua, ni pamoja na homa ya mapafu, kushindwa kupumua, shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari.

Kwa taratibu za kimatibabu ugonjwa ambao mgonjwa huwa anakuwa nao muda mfupi au saa chache kabla ya kifo chake, ndio huwa unatajwa kwenye cheti cha kifo kama sababu ya kifo.


Kuzikwa ardhini

Katika wosia wake wa kiroho, hayati Papa Francis alieleza kuwa anatamani kaburi lake lichimbwe ardhini, liwe rahisi bila mapambo, bali na maandishi mafupi tu yanayosomeka: “Franciscus.”

Alielekeza kwamba maziko hayo yasifanywe kwa mbwembwe, bali kwa utulivu na ibada, huku akiongeza kuwa gharama zote za maandalizi hadi maziko zitatolewa na mfadhili maalumu aliyempangia kila kitu, ikiwemo safari ya mwili wake kutoka Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hadi mahali atakapopumzika.

Baba Mtakatifu pia alimkabidhi Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalumu wa Kipapa wa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, utekelezaji wa mapenzi yake hayo ya mwisho, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapumzika katika kanisa hilo alilolipenda na kulitolea sala mara kwa mara.


Aikabidhi roho yake kwa Bikira Maria

Katika wosia wake wa kiroho, Baba Mtakatifu Francis alikiri kuwa maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu ameyakabidhi siku zote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kristo Yesu. Aliandika kwamba anatamani maisha yake ya kibinadamu yapumzike ndani ya Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkuu, akisubiri siku ya ufufuo wa wafu.

“Mahali nilipojisikia nyumbani ni mbele ya Bikira Maria Mtakatifu. Pale nilipopiga magoti kuomba, napenda ndipo pawe safari yangu ya mwisho,” aliandika katika wosia wake huo.


Sala na maombi kwa ajili ya roho yake

Baba Mtakatifu Francis aliwaombea watu wote waliompenda na wanaoendelea kumwombea, akisema anawatakia wote thawabu stahiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kanisa Katoliki duniani kote linatarajiwa kuwa na maombolezo makubwa, huku mamilioni ya waamini wakitarajiwa kufika Vatican kwa ajili ya kutoa heshima zao na kushiriki katika ibada ya maziko ya kiongozi huyo aliyekuwa maarufu kwa msimamo wake wa kuhubiri huruma, udugu na haki kwa wote.


Ujumbe wa Kwaresima 2025

Katika ujumbe wake wa mwisho wa Kwaresima mwaka 2025, Papa Francis alisisitiza umuhimu wa maisha kama safari ya daima ya uongofu, akihimiza watu kuchagua kutembea katika amani na tumaini pamoja na wenzao.​