Papa Francis atoa wito wa “dunia bila silaha za nyuklia”

Muktasari:
Ametembelea eneo lililoathiriwa na bomu la atomiki Nagasaki na baadaye atakwenda eneo jingine lililopata athari hizo, Hiroshima.
Nagasaki, Japan. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameitaka dunia kuachana na silaha za atomiki, inaripoti Redio Sauti ya Ujerumani (DW).
Ametoa wito huo katika hotuba yake mji Nagasaki, Japan, mji ulioshambuliwa kwa mabomu ya nyuklia mwishoni mwa Vita Kuu vya Pili vya Dunia.
"Eneo hili linatufanya kutambua maumivu na maovu ambayo sisi binadamu tunaweza kufanyiana," alisema Papa Francis katika eneo la uwanja wa kumbukumbu ya mabomu ya atomiki mjini Nagasaki.
Kabla ya hotuba yake aliyotoa huku mvua ikinyesha, papa alitoa heshima zake kwa waathirika wa shambulio la Marekani la bomu la nyuklia mwaka 1945 katika mji huo, kusini magharibi kwa Japan, na kuua watu 74,000, wakiwamo maelfu ya Wakatoliki.
"Hapa katika mji huu ambao ulishuhudia athari za maafa ya kibinadamu na mazingira kutokana na shambulio la nyuklia, juhudi zetu kukemea mashindano ya silaha hazitatosha," amesema Papa Francis, ambaye jana Jumamosi ameanza ziara yake ya siku nne nchini Japan.
Shambulio la Agosti 9, 1945 katika mji wa Nagasaki, lilikuja siku tatu baada ya shambulio la kwanza la bomu la atomiki lililodondoshwa na ndege ya Marekani aina ya B-29 katika mji wa Hiroshima na kuua watu 140,000.
“Eneo hilo linatufanya tukumbuke machungu na maumivu ambayo sisi binadamu tunaweza kuwasababishia watu wengine,” alisema Papa katika siku yake ya kwanza ya ziara.
Mamia ya watu waliobalia makoti meupe ya mvua walikaa katika mvua kubwa wakisikiliza hotuba hiyo mbele ya picha ya kumbukumbu ya mvulana mdogo akiwa amebeba maiti ya mdogo wake mgongoni mara tu baada ya shambulio hilo.
Papa aliweka shada la maua meupe na kuomba kimyakimya bila kuwa na kizuizi cha mvua.
Kuhusu amani
Kiongozi huyo alizungumzia suala la amani akisema, "moja kati ya kile moyo wa binadamu inachopenda zaidi ni usalama, amani na uthabiti.”
Akaongeza, “kuwa na silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi si jibu la hisia hizi ambazo moyo wa binadamu unapenda. Kwa kweli kila mara binadamu anajaribu kuzuia hilo," alisema Papa mwenye umri wa miaka 82.
"Amani na uthabiti wa kimataifa haulingani na majaribio ya kujenga juu ya hofu ya uharibifu wa pamoja au kitisho cha maangamizi ya jumla," amesema.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutia saini na kuidhinisha mkataba wa kuzuia silaha za nyuklia, ambao uliidhinishwa na mataifa 122 Julai 2017.
Hata hivyo, mkataba huo haujaanza kutumika kwa kuwa haujaidhinishwa na mataifa 50 ambayo yanatakiwa kutia saini.
Wanaharakati wa kupinga silaha za nyuklia wameitaka Japan, nchi pekee ambayo imeathirika na mashambulizi ya silaha za atomiki, kutia saini na kuidhinisha mkataba huo haraka iwezekanavyo.
Lakini serikali ya Waziri mkuu Shinzo Abe hadi sasa imekataa kufanya hivyo.
Wakati nchi hizo bado zinasuasua kutia saini, Papa amesisitiza, "nikiwa naamini kuwa dunia bila silaha za nyuklia inawezekana na ni muhimu, nawataka viongozi wa kisiasa kutosahau kuwa silaha hizi haziwezi kutulinda kutokana na kitisho cha hivi sasa katika usalama wa kitaifa na kimataifa.
"Tunahitaji kutafakari athari za maafa ya uwepo wake, hususan kutokana na mtazamo wa kiutu na mazingira na kukataa kuongeza hofu ya kimazingira, kutokuaminiana na uhasama unaochochewa na nadharia za nyuklia".
Papa atafanya ibada ya misa katika uwanja wa michezo mjini Nagasaki baadaye mchana na kisha atasafiri kwenda Hiroshima, ambako mkutano kwa ajili ya amani umepangwa kufanyika.