Papa Francis achagua kuzikwa nje ya Vatican

Muktasari:
- Papa Francis amechagua kuzikwa katika Kanisa la Santa Maria Maggiore ambapo atakuwa papa wa kwanza kuzikwa nje ya Vatican kwa zaidi ya miaka 100.
Vatican City. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amechagua kuzikwa katika kanisa moja huko Roma na siyo kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro pamoja na watangulizi wake kama ilivyo desturi.
“Mahali pameshatayarishwa. Ninataka kuzikwa huko Santa Maria Maggiore,” papa, ambaye anatimiza umri wa miaka 87 wikendi hii, alikiambia kituo cha utangazaji Mexico cha Televisa N+ na kunukuliwa na AFP.
Katika mahojiano hayo, alibainisha kuwa amepanga kutembelea Ubelgiji mwaka 2024, na pia anatarajia kutembelea nchi yake ya Argentina na Polynesia.
Uamuzi wa Papa Francis unamaanisha kuwa atakuwa papa wa kwanza kuzikwa nje ya Vatican kwa zaidi ya miaka 100.
Papa wa mwisho kukwepa kuzikwa katika kanisa la Mtakatifu Petro alikuwa Papa Leo XIII, ambaye alikufa mwaka 1903. Mabaki yake yapo katika kanisa la Mtakatifu John huko Roma.
Santa Maria Maggiore ni moja ya makanisa manne ya kipapa huko Roma, ambalo Papa Francis amesema anahisi uhusiano maalum na kanisa hilo.
Mara nyingi alikuwa akienda huko siku za Jumapili alipokuwa akitembelea Roma kabla ya kuwa papa. Tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, anasali huko kabla na baada ya kusafiri, pia amesali huko baada ya kufanyiwa upasuaji.
Hapo awali, mapapa saba wamezikwa katika kanisa hilo, kwa mujibu wa chombo cha habari cha Vatican News.
Papa amekuwa akikabiliwa na kudhoofika kiafya katika miaka ya hivi karibuni, na alilazimika kukatiza ziara ya majadiliko katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ya COP28 huko Dubai, kutokana na ugonjwa unaomsumbua.
Katika mahojiano yake yaliyorekodiwa Jumanne iliyopita, ambapo alionekana amepata nafuu, alitoa pongezi kwa mtangulizi wake Papa Benedict XVI kwa kuwa na ujasiri wa kujiuzulu wakati afya yake ilipokuwa ikidhoofika.
Papa huyo kutoka Ujerumani, mwaka 2013 alikuwa papa wa kwanza tangu zama za kati kujiuzulu.
Papa Benedict alifariki Desemba 31, 2022, na baada ya mazishi katika kanisa la Mtakatifu Petro huko Vatican, yaliyoongozwa na Papa Francis, mwili wake ulizikwa kwenye kaburi chini ya kanisa hilo.
Ni kaburi lilelile lililohifadhi mwili wa aliyekuwa Papa John Paul II kabla ya kuhamishwa kwa ajili ya kutangazwa kuwa mwenye heri mwaka 2011.
Papa Francis amesema atakuwa tayari kufuata mfano wa Papa Benedict ikiwa hataweza tena kutekeleza majukumu yake, lakini amesema kuachia ngazi kusiwe jambo la kawaida kwa mapapa.