Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Francis ateua maaskofu wawili Tanzania

Muktasari:

  • Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisco amewateua mapadri wawili kuwa maaskofu katika majimbo Katoliki ya Njombe na Bukoba.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisco amewateua mapadri wawili kuwa maaskofu katika majimbo Katoliki ya Njombe na Bukoba.

Maaskofu hao wateule ni pamoja na; Padri Jovitus Mwijage kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba na Padri Eusebio Kyando kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe.

Katika taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Vatcan leo Alhamisi Oktoba 19, 2023 inasema Papa Francis amemteua Padri Kyando kuwa Askofu wa Jimbo la Njombe ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa msimamizi wa kiroho wa Jimbo hilo.

“Alhamisi Oktoba 19, 2023, Baba Mtakatifu Francisko amemteua  Padri Eusebio Samwel Kyando kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe Tanzania,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) pia limetoa taarifa hizo ikiwamo ya uteuzi wa padre Mwijage ambaye atahudumu katika Jimbo Katoliki la Bukoba kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa askofu wa jimbo hilo, Askofu Desiderius Rwoma.

Askofu Rwoma aling’atuka madarakani Oktoba Mosi, 2022 baada ya kuongoza na kuwafundisha waumini kwa miaka 23 kama Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida na baadaye Jimbo Katoliki la Bukoba hadi anastaafu.

Askofu Rwoma aliteuliwa kuwa Askofu wa Bukoba na Papa Benedicto XVI mwaka 2013 hadi mwaka 2022 baada ya papa Francisco kuridhia ombi lake la kung’atuka katika nafasi hiyo ya kichungaji.

Baada ya kung’atuka kwake, Papa Fransco alimteua Askofu Msaidizi, Methodius Kilaini kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Bukoba.

Padri Mwijage ambaye alizaliwa Desemba 2, 1966 katika Wilaya ya Misenyi iliyopo katika jimbo hilo, anajaza nafasi hiyo kama Askofu mpya wa Bukoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 19, 2023 na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, Padri Mwijage alipata daraja la upadri Julai 20, 1997 jimboni Bukoba.

Padri Mwijage amehudumu katika nafasi mbalimbali za kitume jimboni Bukoba na ndani ya TEC kama Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa.

Hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania (Umawata), mjumbe wa Baraza la Seminari Kuu Tanzania na pia Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa (PMS).

Vilevile, Askofu mteule Mwijage alibahatika kutekeleza dhamana na utume wake kama Paroko-usu katika Parokia ya Mwemage na mwalimu na mlezi wa Seminari Ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki la Bukoba.

Naye, Padre Kyando alizaliwa Machi 7, 1964  huko Njombe na kusoma katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Kizito Mafinga, Jimbo la  Iringa, aliendelea na falsafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustino, Peramiho, Songea.