Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jose Mujica: Rais maskini duniani

Aliyekuwa Rais Jose 'Pepe' Mujica wa Uruguay enzi za uhai wake akiwa nyumbani kwake jijini Montevideo nchini humo. Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mujica ambaye ni Rais wa 40 wa Uruguay alijizolea umaarufu ndani na nje ya mipaka ya Uruguay, alipoliongoza taifa lake kufanya mageuzi ya tofauti na mtangulizi wake, Tabare Vazquez.

Uruguay. Ni nadra kukutana na mtu aliyeongoza mapigano ya msituni akajitokeza hadharani kupambana na mfumo uliopo madarakani kisha kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi.

Anayezungumziwa hapa ni Jose ‘Pepe’ Mujica (89), aliyekuwa Rais wa Uruguay kati ya kati ya mwaka 2010-2015. Kifo cha Mujica kilitangazwa juzi Jumanne na Rais wa nchi hiyo, Yamandu Orsi, kupitia mitandao ya kijamii.

“Ni huzuni kubwa tunatangaza kifo cha kamanda wetu Pepe Mujica. Asante kwa yote uliyotupatia na kwa upendo wako wa dhati kwa watu wako,” aliandika Rais Orsi.

Aliyekuwa Rais wa Uruguay, Jose 'Pepe' Mujica akiwa na mke wake, Lucía Topolansky. Picha na Mtandao.

Mujica ambaye ni Rais wa 40 wa Uruguay alijizolea umaarufu ndani na nje ya mipaka ya Uruguay, alipoliongoza taifa lake kufanya mageuzi ya tofauti na mtangulizi wake, Tabare Vazquez.

Pia, alisifiwa kwa maisha yake ya unyenyekevu hata alipokuwa rais, alipokataa kuishi katika Ikulu ya Rais na kuendelea kuishi kwenye shamba lake alikokuwa akilima maua. Aliliambia Shirika la Al Jazeera mwaka 2022 kuwa anasa kama hizo zinaweza kuwatenga marais na watu wao.

Kwa mujibu wa Yamandu Orsi, kifo cha Mujica kimetokana na ugonjwa wa saratani ya koo.

Aliyekuwa Rais wa Uruguay, Jose 'Pepe' Mujica akiwa kwenye gari yake pendwa ya ‘Volkswagen Beetle’ la mwaka 1987. Picha na Mtandao.

Mujica alipewa taarifa ya kuugua saratani Septemba 2024 ambapo madaktari walimueleza kuwa matibabu ya mionzi yamefanikiwa kuondoa saratani hiyo, lakini Januari mwaka huu daktari wake aliripoti  kuwa saratani hiyo ilienea hadi kwenye ini.

"Mimi ninakufa," Mujica alilieleza Gazeti la Busqueda huku akidokeza kuwa mahojiano hayo yatakuwa ya mwisho kwake kufanya kwenye vyombo vya habari.

“Shujaa ana haki ya kupumzika,” Mujica alisema.
 

Alikuwa muasi

Mujica, aliyejizolea umaarufu nchini Uruguay kwa jina la utani, "Pepe," akiwa na umri wa miaka 8 baba yake alifaiki na jukumu la kumlea kubakia mikononi mwa mama yake ambaye wakati huo alitegemea biashara ya kuuza maua.

Huku akikerwa na uwepo wa tabaka kubwa kati la wenye mali na maskini nchini Uruguay, alijikuta akivutiwa uanaharakati na Mapinduzi ya Cuba ya 1959, alitafuta mabadiliko ya kisiasa kupitia vita vya msituni.

Akiwa kijana katika miaka ya 1960, Mujica alijiunga na kundi la National Liberation Movement, kundi la ‘waasi’ lililojulikana sana kama ‘Tupamaros’. Wanachama wake walifanya uhalifu na matukio mengi ikiwemo kulipua mabomu, wizi wa benki na utekaji nyara. Mwaka 1969 waliteka mji wa Uruguay wa Pando.

Hata hivyo kundi hilo la Tupamaro halikufanikiwa kutwaa madaraka wala kupindua serikali.

Mnamo mwaka 1970, Mujica akiwa ni mwanachama wa genge hilo, alikamatwa katika tukio linalohusisha kurushiana risasi na polisi nchini Uruguay. Katika tukio hilo Mujica alijeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Baada ya kutibiwa, Mujica alishtakiwa na kufungwa jela na wafungwa wenzake wa Tupamaros. Akiwa jela na wafungwa wenzake walijenga handaki lenye urefu wa futi 130 hadi nyumba moja pembeni mwa barabara iliyopo karibu na gereza hilo, jambo ambalo lilimpa nafasi Mujica na waasi wengine 105 kutoroka na baadhi walikamatwa.

Baada ya jaribio hilo la kutoroka kugonga mwamba, Mujica alipigwa na kuteswa, na alitumia muda mwingi katika kifungo cha upweke hadi akafanya urafiki na wadudu wakiwemo mchwa, vyura na panya.

Hakika, ghasia za waasi na machafuko yalidhoofisha Serikali ya kiraia ya Uruguay na kuchangia kutokea mapinduzi ya 1973 ambayo yaliiingiza nchi hiyo katika utawala wa Kidikteta chini ya jeshi.

Mujica aliachiwa mwaka 1985. Kufikia wakati huo, utawala wa kidikteta wa Uruguay ulikuwa umetoa nafasi kwa Serikali ya kidemokrasia na hatimaye Mujica akakubali kuingia katika siasa.

Alianza kuwa na nguvu katika siasa za Uruguay, akajiunga na chama cha Frente Amplio ama Broad Front, muungano wa mrengo wa kati na wapiganaji wengine wa zamani.


Safari ya kisiasa

Alichaguliwa kuwa mbunge wa bunge la nchi hiyo mwaka 1994, akateuliwa kuwa Waziri wa Mifugo, Kilimo na Uvuvi mwaka 2005. Baada ya miaka minne bungeni, Mujica alijitosa kuwania urais kupitia chama chake na kushinda kwa kishino.

Katika utawala wake, Mujica alijikita kuleta mageuzi kwenye sekta ya mazingira na kulegeza masharti kwenye matumizi ya bangi. Rais huyo pia alikuwa balozi mzuri wa matumizi ya nishati safi jambo lililoifanya Uruguy kuwa kinara wa kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Katika utawala wake, Mujica alipambana kupunguza kiwango cha umaskini kwa wananchi wake huku akijiepusha na tabia zinazohusiana na ubadhirifu wa mali ya Umma. Wakati wa utawala wake, Uruguay ilikuwa taifa lililoongoza kwa kutoa hifadhi kwa wakimbizi wa kimataifa hususan mataifa ya Mashariki ya Kati ikiwemo Syria na Afghanistan.

Mwandishi wa Kitabu cha ‘The Robin Hood Guerrillas’, kinachoeleza historia ya Mujica, Pablo Brum aliwahi kunukuliwa akisema; "Ulikuwa urais wenye mafanikio makubwa.”

Familia

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, Mujica, alifunga ndoa mwaka 2005 na mpenzi wake wa muda mrefu, Lucía Topolansky, ambaye pia alikuwa mwanachama wa zamani wa kundi la Tupamaros, baada ya kuishi pamoja kwa miaka mingi.

Tangu wakati huo wafunge ndoa, Mujica na mkewe, Topolansky hawakubahatika kupata mtoto. Hata hivyo, hilo halikuwavunja moyo, walindeleza upendo wao. Amemwacha mkewe Topolansky akiwa na umri wa miaka 80.

Wawili hao, hawakuwa na watoto na waliishi katika shamba la Topolansky lililoko eneo la pembeni la Jiji la Montevideo, ambako walikuwa wakilima maua aina ya ‘Chrysanthemum’ na kuyauza.

Wapenzi hao walipendelea kufuga wanyama wakiwemo mbwa wao pendwa, anayeitwa Manuela. Mbwa huyo alikuwa na miguu mitatu.

Topolansky alihudumu kwa muda kama Kaimu Rais, Novemba 2010 wakati mumewe alipokuwa katika ujumbe wa kibiashara nchini Hispania na Makamu wa Rais wa wakati huo, Danilo Astori, alipokuwa katika safari rasmi bara la Antaktika. Kabla ya hapo, aliwahi kuhudumu katika Bunge la Wawakilishi na Seneti.


‘Rais maskini zaidi’

Mujica alikataa kuishi katika jumba la Rais ama kutumia wafanyakazi wake wakati wa urais wake. Kwa wakati wote alitumia gari yake pendwa ya ‘Volkswagen Beetle’ la mwaka 1987 na baiskeli yake ya miaka 60 alipotaka kusafiri.

Mwaka wa 2010, thamani ya gari hilo ilikuwa dola za Marekani 1,800 (Sh4.8 milioni) na hiyo ndiyo ilikuwa taarifa yake yote ya mali binafsi aliyowasilisha kwa mwaka huo.

Alivaa kawaida na alitoa karibu mshahara wake wote kwa misaada. Maisha yake ya kawaida yaliwafanya wengine kumwita ‘Rais maskini zaidi duniani’.

“Tunamchagua rais, na siYo mfalme anayetaka zulia jekundu na kuishi katika jumba la kifahari," amesema mwaka 2022.

Mujica alikuwa mtu mashuhuri kwa umma hata baada ya kuacha urais, akihudhuria hafla ya kuapishwa kwa viongozi wa kisiasa kote Amerika ya Kusini.

Novemba 2014, gazeti la Uruguay la Búsqueda liliripoti kuwa alipewa ofa ya dola za Marekani 1,000,000(zaidi ya Sh2.6 bilioni) kwa ajili ya gari hilo, hata hivyo, Mujica alisema kuwa kama angepokea pesa hizo, angezitoa kusaidia mpango wa kuwapatia makazi wasio na makazi, ambao alikuwa akiunga mkono.

Aliyekuwa Rais wa Uruguay, Jose 'Pepe' Mujica akiwa kwenye gari yake pendwa ya ‘Volkswagen Beetle’ la mwaka 1987. Picha na Mtandao.

‘Sina dini’

Katika mahojiano yake na BBC, Novemba 2012, Mujica alisema, “Sina dini,”. Katika barua aliyomtumia Rais wa Venezuela wakati huo, Hugo Chávez, Desemba 2012 akimtakia kupona haraka, alieleza wazi kuwa japokuwa yeye si muumini, angeomba misa ifanyike kwa ajili yake.

 Mujica na Topolansky hawakuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Papa Francis mwaka 2013. Topolansky alieleza kuwa kutokuwepo kwao kulitokana na kuwa wao “si waumini”.

Astori, ambaye alikuwa Mkatoliki, alihudhuria kwa niaba yao. Kauli hizi zilipelekea vyombo vya habari kumchukulia Mujica kama mmoja wa marais wawili pekee waliotangaza wazi kuwa hawana dini katika bara la Amerika Kusini, pamoja na Raúl Castro wa Cuba.

Shabiki wa Club Atletico Cerro

Mujica alikuwa shabiki mkubwa wa mchezo wa kandanda na aliunga mkono klabu ya nyumbani ya Club Atlético Cerro.

Hata timu ya Uruguay iliporejea kutoka  Kombe la Dunia mwaka 2014 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Carrasco, na baada ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kumsimamisha, Luis Suárez wa Uruguay kushiriki shughuli zote za soka kwa miezi minne kwa kumng’ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini, Mujica aliikosoa Fifakwa vikali, akiita viongozi wake huku akisema kuwa walitoa adhabu ya kifashisti.

Alipogundua kuwa alikuwa akirekodiwa, Mujica aliziba mdomo wake. Waandishi wa habari walimuuliza kama wangeweza kuchapisha kauli yake, naye alijibu kwa kicheko ‘ndiyo’.


Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.