Netanyahu azidi kutangaza mapigano, atakiwa kujiuzulu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Gaza. Zikiwa zimetimia siku 82 tangu kuzuka mapigano kati ya Israel na Hamas, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ametangaza mapambano zaidi baada ya vifo vya wanajeshi wa Taifa hilo kuongezeka.
Netanyahu ametoa kauli hiyo wakati mashambulizi ya anga yakiongezeka katika ukanda wa Gaza.
Akizungumza alipotembelea eneo hilo juzi, Netanyahu aliahidi kuzidisha mapigano.
Alisema hawatasitisha mashambulizi, bali vita hivyo vitakuwa virefu.
“Tunaongeza mapambano katika siku zijazo, na hivi vitakuwa vita virefu,” alikaririwa Netanyahu na Shirika la Utangazaji la VOA.
Hata jana zaidi ya watu 100 walikuwa wameuawa katika shambulizi la anga la Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Maghazi, baadhi ya familia bado zimenasa kwenye vifusi.
Mamlaka ya Palestina imeripoti watu 250 wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi yaliyofanywa na Israel ndani ya saa 24 katika Sikukuu ya Krismasi.
Israel imesema wanajeshi wawili wameuawa na kufanya idadi ya waliouawa eneo la Gaza hadi juzi kufikia 158.
Ripoti zaidi zinasema Misri inapendekeza mpango wa kumaliza mzozo wa sasa kwa kusitisha mapigano, kuachiliwa mateka kwa awamu na kuundwa kwa Serikali ya Palestina.
Hata hivyo, hakuna jibu rasmi kutoka kwa Israel au Hamas kutokana na pendekezo hilo.
Wito Netanyahu ajiuzulu
Shirika la Habari la Al Jazeera limemkariri kiongozi wa upinzani wa Israel akisema Netanyahu hawezi kuendelea kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Kiongozi huyo, Yair Lapid alisisitiza wito wa kumtaka Netanyahu kujiuzulu.
“Kubadilisha uwaziri mkuu katikati ya vita si vizuri. Lakini aliye madarakani ni mbaya zaidi. Hawezi kuendelea,” alisema.
Inaelezwa Lapid alikataa kujiunga na baraza la mawaziri la Netanyahu mwanzoni mwa vita vya Israel na Hamas na amekuwa mkosoaji wa mara kwa mara wa Serikali ya Netanyahu.
WHO yaonya njaa
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya juu ya hatari ya kuongezeka njaa katika eneo linalopiganiwa la Gaza.
WHO imesema hakuna chakula wala nishati ya kupikia.
“Njaa imeukumba ukanda wa Gaza kwa mujibu wa WHO, hivyo kutishia ongezeko la magonjwa, hasa kwa watoto, wajawazito na wanaonyonyesha na makundi mengine yaliyo hatarini. Nishati ya kupikia nayo hakuna,” inaeleza taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN).
Shirika hilo limeonya kwamba Gaza inakabiliwa na viwango vikubwa vya ukosefu wa chakula.
Kwa mujibu wa WHO, kuna wagonjwa zaidi ya 100,000 wa kuhara eneo la Gaza tangu katikati ya Oktoba, mwaka huu.
Inaelezwa kuwa nusu ya wagonjwa hao ni watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.
Pia, kuna wagonjwa zaidi ya 150,000 wa maradhi ya mfumo wa hewa, uti wa mgongo, upele na tetekuwanga.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef) limesema watoto na familia katika ukanda wa Gaza wanakabiliwa na ghasia kutoka angani na ardhini, huku kukiwa na uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi.
Unicef imesema takribani watu milioni 1.2 wanakabiliwa na uhaba wa chakula.
“Hii inaashiria kuwa watoto wote walio chini ya miaka mitano katika ukanda wa Gaza wako katika hatari ya utapiamlo mkali na vifo vinavyoweza kuzuilika,” inaeleza Unicef.
Pia, inakadiria katika wiki zijazo, takribani watoto 10,000 walio chini ya miaka mitano watapata utapiamlo.
Kwa jumla mashirika ya Umoja wa Mataifa yanashinikiza usitishaji mapigano wa haraka ili misaada ya kibinadamu kuwafikia walengwa na kuwezesha huduma muhimu kupatikana ukanda wa Gaza.
Hatua hiyo itaruhusu watoto walio katika mazingira magumu kukidhi mahitaji yao ya kimsingi ya lishe na afya, ikiwa ni pamoja na kupatiwa maziwa, chakula na virutubisho vya lishe.
“Tunahitaji kurejeshwa kwa miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na hospitali ili watoto wadogo, wajawazito na majeruhi waweze kupata matibabu na huduma za kuokoa maisha kwa usalama,” inaeleza taarifa ya Unicef.