Mauzo ya magari ya umeme yashamiri
Paris, Ufaransa (AFP)
Kiwango cha magari ya umeme kimeongeza zaidi ya mara mbili katika mauzo ya magari mapya barani Ulaya katika robo ya pili ya mwaka, huku ya nishati mseto pia yakishamiri, Chama cha Watengeneza Magari Ulaya (ACEA) kimesema leo Ijumaa.
Idadi ya magari yote ya umeme ilikuwa ni asilimia 7.5 ya mauzo ya magari mapya barani Ulaya katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni, ikiwa ni tofauti na kiwango cha asilimia 3.5 kwa kipindi kama hicho mwaka jana.
Kwa ujumla, magari yanayotumia betri ya umeme yalipanda mara tatu zaidi kote barani Ulaya hadi kufikia magari 210,298.
ACEA ilisema kulikuwa na ongezeko kubwa katika eneo la masoko manne makuu, likiongozwa na Hispania na Ujerumani ambako mauzo yalikuwa mara nne zaidi.
"Magari ya nishati mseto- yanayotumia umeme na mafuta--(Plug-in hybrid electric vehicles, PHEVs) pia yalikuwa na mauzo mazuri katika robo ya pili ya mwaka 2021, huku usajili ukipanda kwa asilimia 255.8 hadi kufikia magari 235,730," ilisema ACEA.
Mauzo ya magari ya nishati mseto yalipanda zaidi ya mara tatu hadi kufikia magari 541,162, ikiendelea kuwa kiwango kikubwa cha mauzo ya magari ya nishati mbadala.
Wakati huohuo, usajili wa magari mapya yanayotumia petroli na dizeli uliongezeka kwa kuangalia idadi ndogo ya magari yaliyouzwa katika robo ya pili mwaka jana, wakati nchi nyingi za Ulaya zilipokuwa na masharti makali ya biashara kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya corona.
Lakini kwa kuangalia mgawanyo wa soko, mauzo ya magari yote ya petroli na dizeli yalishuka kwa kiwango kikubwa.