Kenya yashindwa kulipa wafanyakazi, Ruto asema hakopi

 Rais wa Kenya, William Rutto.

Muktasari:

  • Rais wa Kenya, William Ruto amesema Serikali yake haitakopa ili kupata fedha za kuwalipa wafanyakazi wake kufuatia kukosa hela za mishahara kuwalipa watumishi wake.

Kenya. Rais wa Kenya, William Ruto amesema nchi hiyo haitakopa ili kuwalipa wafanyakazi wa umma hata baadhi ya vyama vya wafanyakazi kutishia kugoma kutokana na kutolipwa mishahara ya Machi.

Ruto alilaumu ucheleweshaji wa deni kubwa la umma nchini humo, kutokana na baadhi ya mikopo ambayo inatakiwa mwezi huu.

Alisema mishahara ya wafanyakazi ambao bado hawajalipwa italipwa kutokana na ushuru unaokusanywa na mamlaka ya mapato nchini humo.

Mpaka sasa mashirika mawili ya wafanyakazi yametoa vitisho vya kugoma wiki hii ikiwa wafanyakazi wake hawatalipwa mishahara yao.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Jumatatu Aprili 11, 23023, mshauri mkuu wa marais wa masuala ya kiuchumi alisema mishahara hiyo italipwa hadi mwisho wa mwezi lakini akashauri Serikali kupunguza ufujaji wa fedha za umma.

Deni la Kenya sasa linafikia asilimia sitini na tano ya mapato yote ya nchini humo.

Kenya inahitaji zaidi ya Dola 420 milioni kila mwezi kulipa mishahara na pensheni kwa watumishi wa umma.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Benki ya Dunia na IMF kutoa onyo tofauti kwamba nchi za Kusini mwa Afrika zinakabiliwa na mgogoro mpya wa madeni, huku nchi nyingi zikiwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na madeni.

Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua alithibitisha kuchelewa kwa mishahara ya wafanyakazi wa Serikali na kutumwa kwa pesa katika kaunti mbalimbali kutokana na uhaba wa fedha unaolikabili taifa hilo.

Akizungumza katika ibada ya kanisani huko Mathira katika Kaunti ya Nyeri, Gachagua alisema kuwa uhaba wa fedha umeletwa na Serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Rais William Ruto alirithi nchi hii kutoka kwa Uhuru Kenyata ikiwa haina kitu. Ukweli ni kwamba Rais Ruto alianza moja kujenga uchumi wa Nchi hii,” alisema Gachagua.

Kwa mujibu wa Makamu huyo wa Rais, Serikali ya Uhuru ilifilisi kabisa hazina ya Taifa kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kifedha.

"Ni kweli tuna shida ya kulipa mishahara na kutuma pesa kwa kaunti kwa sababu utawala wa handshake (maridhiano) ulilamba kila kitu. Kila kitu kimeisha," alisema Gachagua.

Maelfu ya wafanyakazi katika kaunti zote 47 wameishi kwa miezi kadhaa sasa bila kupokea mishahara yao baada ya Serikali ya kitaifa kukosa kulipa fedha kwa wakati.

Hazina ya Kitaifa ya nchini humo bado haijalipa Sh96 bilioni za miezi ya Januari, Februari na Machi na kuwaacha wafanyakazi wa kaunti wakilaumu serikali.

Serikali za kaunti zimekua zikishinikiza Serikali kuu kuwapatia fedha kwa wakati ili kulipa mishahara na kuepeka migomo ambayo tayari baadhi ya wafanyakazi wake wameanza kutishia kugoma kufanya kazi


Imeandaliwa na Victor Tullo.