Israel yabadilishana wafungwa kwa mateka

Muktasari:
- Shirika la Habari la Uingereza (BBC), limeripoti kuwa wafungwa hao waliachiliwa jana Ijumaa Novemba 24, 2023 kama sehemu ya makubaliano yaliyosimamiwa na Qatar, huku yakijumuisha usitishwaji wa mapigano kwa siku nne.
Dar es Salaam. Jumla ya wafungwa 39 wa Kipalestina waliokuwa wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini Israel, wameachiwa huru katika mpango wa kubadilishana wafungwa, mateka baina ya wanamgambo wa Hamas na Israel.
Shirika la Habari la Uingereza (BBC), limeripoti kuwa wafungwa hao waliachiwa jana Ijumaa Novemba 24, 2023 kama sehemu ya makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Qatar, huku yakijumuisha usitishwaji wa mapigano kwa siku nne.
Imeripotiwa kuwa wanawake 24 na vijana wa kiume 15, walitolewa katika magereza ya Beituniya Magharibi mwa Israel na inadaiwa wataruhusiwa kurudi nyumbani, kulingana na maofisa wa Israeli.
Wafungwa hao walichaguliwa kutoka katika orodha ya wanawake na watoto 300 iliyoandaliwa na Israel huku wengi wao wanashikiliwa rumande wakisubiri kesi zao kusikilizwa.
Wengi wa walioorodheshwa ni vijana wa kiume chini ya miaka 18, pia kuna msichana mmoja na wanawake 32.
Makundi ya wanaume na wavulana wa Kipalestina yalikabiliana na jeshi la Israel lililojipanga barabarani huku askari wake wakifyatua risasi za mpira na mabomu ya machozi kuelekea umati wa watu, ili kuwarudisha nyuma na vijana waliokusanyika walijibu mashambulizi hayo kwa kuwarushia mawe askari hao.
"Ni ishara ya matumaini kwa Wapalestina na Waisraeli kwamba usitishaji vita utaendelea na mauaji yatakoma," Mohammed Khatib, ambaye alikuwa katika umati huo, aliiambia BBC.
Wakiwa ndani ya basi, baadhi ya wafungwa hao walionekana kupitia madirishani, wakicheza kufurahia kuachiwa huru, huku mmoja akiwa amejifunga bendera ya Palestina.
Kwa upande mwingine, mateka 13 wa Israel ambao ni sehemu ya wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas, pia waliachiwa huru chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, huku ikithibitishwa jana kuwa walikuwa wamerejea nchini Israeli.
Waziri Mkuu wa Thailand amesema kuwa kundi la raia wa nchi yake waliokuwa wametekwa na Hamas huko Gaza, pia waliachiwa.
Israel na Hamas zilifikia makubaliano mapema wiki hii ya kuwaachilia mateka 50 walioshikiliwa huko Gaza wakati wa usitishwaji mapigano kwa siku nne.
Mkataba huo unapaswa kuona jumla ya Wapalestina 150 wanaoshikiliwa katika jela za Israel wakiachiwa huru, huku kipindi hicho pia kikitumia kutoa ruhusa ya kuongeza misaada ya kibinadamu Gaza.
Imeelezwa kuwa baadhi ya malori 60 yakiwa na vifaa vya matibabu, mafuta na chakula yaliingia Ukanda wa Gaza kutoka Misri jana Ijumaa.
Hamas iliwachukua mateka zaidi ya watu 200 wakati wa shambulio la kuvuka mpaka Kusini mwa Israel Oktoba 7, 2023, ikidaiwa kuwa watu 1,200 waliuawa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa idadi ya Wapalestina wanaoshikiliwa bila kufunguliwa mashtaka katika jela za Israel imeongezeka tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.
Kwa sasa inakisiwa kuwa zaidi ya Wapalestina 6,000 wanaoshikiliwa na Israel kwa misingi ya usalama huku wengi wao bado wanasubiri kuhukumiwa.
Takriban kila familia ya Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi inadhaniwa kuwa na jamaa anayeshikiliwa nchini Israel.