Afariki dunia akiwasaidia bata kuvuka barabara

Muktasari:

  • Mtu mmoja kutoka California amefariki baada ya kugongwa na gari wakati akiwasaidia bata kuvuka barabara polisi wa eneo hilo wamesema.

California. Mtu mmoja kutoka California nchini Marekani amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akiwasaidia bata kuvuka barabara, polisi wa eneo hilo wamesema.

 Casey Rivara (41) aliacha gari lake na kuwavusha bata waliokuwa wanavuka barabara kabla ya kugongwa na gari lililokuwa linaendeleshwa na dereva kijana huko Rocklin, yapata maili 25 (40km) kaskazini mashariki mwa Sacramento.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema Rivara kabla ya kupata ajali ajali hiyo alihakikisha bata hao wamevuka salama barabara kabla ya kugongwa na gari.

"Mwanamume huyo alikuwa anawasaidia watoto wa bata ambao walikuwa wakivuka kwenye makutano ya barabara, ndipo dereva kijana ambaye alikuwa akielekea upande wa mashariki kwenye Stanford Ranch Boulevard, alimgoga," idara ya Polisi ya Rocklin imesema katika taarifa yake kwa umma.

Ndugu wa marehemu wamesema Rivala alikuwa akiwarudisha watoto wake nyumbani baada ya mazoezi yao ya kuogelea ndipo walipomwona bata na watoto wake wakihangaika kuvuka katika makutano ya barabara.

"Casey alikuwa mume na baba mkarimu zaidi, mzuri zaidi, hata kitendo chake cha mwisho hapa duniani kilikuwa ishara ya huruma yake,” alisema ndugu wa marehemu.

Mjane wake, Angel Chow, alisema katika taarifa yake: "Tunataka kutoa shukrani zetu za dhati kwenu nyote kwa salamu za pole na matendo ya huruma kwetu.

Idara ya Polisi ya Rocklin ilisema hakuna mtu aliyekamatwa na tukio hilo bado linachunguzwa.

Kapteni wa Polisi wa Rocklin Scott Horrillo aliambia NBC News kwamba dereva huyo atakabiliwa na mashtaka ya uhalifu.