Serikali yaja na mradi wa kuhifadhi maziwa madogo
Muktasari:
- Maziwa hayo ni pamoja na Ziwa Rukwa (Rukwa), Natron na Eyasi (Arusha), Jipe na Chala (Kilimanjaro) na Manyara lililopo katika Mkoa wa Manyara.
- Sambamba na maziwa hayo, mito ya Wami na Pangani nayo iko hatari kutoweka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu.
Baadhi ya maziwa yaliyopo katika mikoa mbalimbali nchini yako hatarini kutoweka kwa sababu tofauti ikiwamo watu kuvamia vyanzo vyake kwa kufanya shughuli za kibinadamu kandokando ya maziwa hayo.
Maziwa hayo ni pamoja na Ziwa Rukwa (Rukwa), Natron na Eyasi (Arusha), Jipe na Chala (Kilimanjaro) na Manyara lililopo katika Mkoa wa Manyara.
Sambamba na maziwa hayo, mito ya Wami na Pangani nayo iko hatari kutoweka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu.
Kuvamiwa maziwa na mito hiyo kunahatarisha uhai wa rasilimali ambazo ni muhimu kwa ajili ya maisha ya binadamu na ustawi wa nchi.
Ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliyoifanya mikoa ya Tanga, Arusha, Pwani na Kilimanjaro imebaini kwamba shughuli za kibinadamu ndicho chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira katika mito na maziwa hayo.
Septemba mwaka jana, Makamba alifanya ziara ya kukagua shughuli za utunzaji mazingira katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Morogoro, Mbeya, Iringa, Katavi, Rukwa na Songwe na kukutana na uharibifu wa mazingira hasa katika Mto Katuma ambao watu walivamia chanzo cha maji cha Ziwa Rukwa na wafugaji wanapeleka mifugo yao ziwani.
Katika ziara ya hivi karibuni, Makamba alikumbana na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira, mfano katika Ziwa Jipe lililopo Kata ya Butu wilayani Mwanga wakulima wanalima kandokando yake, jambo linalosababisha kushamiri kwa magugu maji.
Ziwa hilo linapakana na nchi ya Kenya, lakini upande wa Tanzania unakabiliwa na magugu maji tofauti na Kenya ambako wameweka utaratibu maalumu wa kudhibiti shughuli za kibinadamu na kuwawezesha kuvua samaki wengi wakubwa.
Pia, Makamba alijionea baadhi ya wafugaji wanaopeleka mifugo yao kandokando ya ziwa hilo jambo linalosababisha uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
Kutokana na hali hiyo, waziri huyo anasema atalitangaza Ziwa Jipe kwenye Gazeti la Serikali kuwa eneo maalumu la hifadhi za mazingira ili kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazofanyika kinyume na sheria na kulinda rasilimali zilizomo ndani yake.
Waziri huyo anawaeleza wakazi wa Butu kwamba, uamuzi huo una lengo la kurejesha ziwa hilo katika hali yake ya zamani lengo likiwa ni kuendelea kuwasaidia kiuchumi wakazi wa eneo hilo wengi wao wakiwa wanaotegemea uvuvi kwa ajili ya kipato.
“Magugu maji haya yanasababishwa na shughuli za kilimo mnazozifanya kandokando ya ziwa kwa sababu mbolea mnayotumia inachangia moja kwa moja kushamiri kwa magugu maji haya sanjari na kuchafua maji,” anasema.
Uamuzi wa Makamba kulifanya ziwa hilo kuwa eneo la hifadhi ya mazingira umepokewa kwa furaha na wakazi wa Butu, akiwamo Mkuu wa wilaya hiyo, Aaron Mmbago ambaye alimuahidi waziri huyo kuwa atahakikisha Ziwa Jipe linalindwa kwa kushirikiana na viongozi husika.
Kuhusu Ziwa Natron, Makamba anasema wananchi hajawalivamia kutokana na kuwa na magadi, lakini kiwango cha maji kimepungua hivyo ataagiza timu ya wataalamu kufanya utafiti ili kujua kinachosababisha hali hiyo.
Waziri huyo anasisitiza kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kuyalinda maziwa hayo kwa kuweka mikakati ambayo itawezesha rasilimali hizo kurudi katika ubora wake.
Mikakati ijayo
Makamba anasema Serikali ipo katika mchakato wa kubuni mradi wa kuhifadhi maziwa madogo nchini ili kuhakikisha kwamba yanarudi katika hadhi yake.
Anasema mradi huo mkubwa wa kitaifa wa Serikali utashirikisha washirika wa maendeleo wa kimataifa katika kuhakikisha maziwa yanalindwa na kuhifadhiwa vizuri.
Makamba anafafanua kuwa mradi huo umejikita kuwapa mbinu na shughuli mbadala wananchi walio kandokando ya maziwa hayo ili waachane na fikra ya kutegemea rasilimali hizo kama sehemu ya kujingizia kipato.
Anatoa mfano wa baadhi ya wakazi wa Kilolo mkoani Iringa ambao walivamia vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo hali iliyosababisha maji yasifike kwa utaratibu unaotakiwa katika maeneo mbalimbali hasa kwenye Bwawa la Kufua Umeme la Kihansi.
Anasema katika kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri, Serikali ilikuja na mkakati uliosaidia kuondoa hali hiyo.
“Serikali iliamua kuwapa mradi wa ufugaji nyuki ambapo tuliwapa mizinga ya kufugia nyuki wao na waliachana na tabia ya kuvamia vyanzo vya maji,” anasema Makamba.
Waziri huyo anasema kuwa njia hiyo ni mojawapo inayoweza kutumika kwa baadhi ya wananchi wanaozunguka na kuishi kandokando ya maziwa hayo sita.
Mbali na hilo, Makamba anasema mfano Serikali inaweza kufikiria kuweka utaratibu maalumu wa kuwawezesha wananchi kufuga bila kufanya uharibifu wa mazingira kwenye maziwa hayo au vyanzo vya maji.
Anasema kuwa, tayari wizara yake imeshaiagiza timu ya wataalamu kwenda katika maeneo hayo kwa ajili ya kufanya utafiti, kisha kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mradi huo.
“Kuhusu fedha za kuendesha mradi huu, mimi najua wapi zitapatikana. Tunasubiri wataalamu wakamilishe kuandaa mpango huo,” anasema Makamba na kuongeza kuwa kila ziwa lina changamoto zake ikiwamo baadhi kupakana na nchi jirani hasa ya Kenya.
Hata hivyo, anasema mchakato huo utawahusisha wananchi wa maeneo husika ikiwamo kuwapa elimu ya jinsi mradi utakavyotekelezwa pamoja na faida zake.
Anasema Serikali inajua kwamba asilimia kubwa ya wakazi wanaozunguka maziwa hayo wanayategemea kuendesha maisha yao na kwamba, ni vyema wakashirikishwa kikamilifu katika mradi wa kuyahifadhi.
Makamba anasisitiza kuwa mradi huo utahusisha ustawi wa watu wanaoishi na kuzunguka maziwa hayo ikiwamo maendeleo yao: “Ili watu waone kama kwamba kuna manufaa ya uhifadhi, lazima wanufaike na uhifadhi,” Makamba aliwaambia wakazi wa kijiji cha Engaresero wilayani Ngorongoro
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka anasema uamuzi huo wa Serikali ni jambo jema kwa uhifadhi wa maziwa madogo likiwamo la Natron ambalo liko katika wilaya anayoiongoza.
“Uzuri wa wananchi wa Ngorongoro walishaanza uhifadhi siku nyingi, kwa hiyo utaratibu huu ukianza hawatapa shida. Tuko tayari kufungua macho na masikio katika mradi huu wa aina yake ili kuhifadhi maziwa,” anasema Taka.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Mmbago anasema ni mradi mzuri kwa sababu una lengo la kusaidia kuhifadhi maziwa sita ili kuyarudishia uhalisia wa awali.
“Uamuzi na njia zitakazotumika ni sahihi kwa sababu wananchi watapatiwa shughuli mbadala za kufanya badala ya kuendelea kutegemea maziwa haya,” anasema Mmbago.
Anasema kuwa wanausubiri kwa hamu mradi huo na wananchi watashirikishwa kikamilifu, na kwamba uamuzi huo utakuwa tofauti na ule wa kufungwa kwa Bwawa la Nyumba Mungu.
“Baada ya kufungwa (kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu) wananchi walilamikia uamuzi huo kwa sababu hawana shughuli za kufanya, kwa madai kwamba bwawa lilikuwa tegemeo lao. Lakini mradi huu uko tofauti kwa kuwa kutakuwa na mbadala wa shughuli,” anasisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Kwa mujibu wa Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga, anasema ziara zake zitakuwa endelevu na mikoa ya Kusini na Magharibi ndiyo itakayofuata ili kuhakikisha uharibifu wa mazingira unatambuliwa na kudhibitiwa.
Makamba anasema bado uharibifu wa mazingira ni mkubwa na anawasisitizia Watanzania umuhimu wa kuyatunza na kuyahifadhi, kwa sababu shughuli za kiuchumi zikiwamo kilimo na ufugaji zinategemea kwa kiasi kikubwa shughuli za uhifadhi mazingira bora.