Wenza wa viongozi wawauma sikio wajasiriamali fursa daraja la JP Magufuli

Umoja wa Wenza wa viongozi (Ladies of New Millenium Women Group) ukisikiliza maelezo ya wajasiriamali wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya masikini (Tasaf) eneo la Shule ya Sekondari Igogwe wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza ikiwa ni ziara yao ya kukagua utekelezaji miradi ya Tasaf.
Muktasari:
- Mwenyekiti wa umoja wenza wa viongozi, Tunu Pinda amewapongeza wanawake kwa jitihada zao za kujikwamua kiuchumi na kuwataka watumie miundombinu inayojengwa na Serikali kufikia masoko zaidi.
Mwanza. Umoja wa wenza wa viongozi wa kitaifa, Ladies of New Millennium Women Group, umewataka wanawake wajasiriamali kutumia daraja la JP Magufuli kupanua biashara zao ndani na nje ya Kanda ya Ziwa.
Rai hiyo imetolewa Juni 25, 2025, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwemo Shule ya Sekondari ya Igogwe na kuwatembelea wanawake walionufaika na ruzuku.
Pia, umoja huo umetoa majiko 25 ya gesi kwa wanawake hao ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mwenyekiti wa umoja huo, Tunu Pinda amewapongeza wanawake kwa jitihada zao za kujikwamua kiuchumi na kuwataka watumie miundombinu inayojengwa na Serikali kufikia masoko zaidi.

“Serikali inajenga barabara na madaraja ili muweze kufikia masoko kwa urahisi. itumieni nafasi hii kupeleka bidhaa zenu sehemu mbalimbali,” amesema Pinda.
Mjumbe wa umoja huo, Hasna Kawawa amesema amefurahishwa na mafanikio ya wanawake hao na kuwasihi waendelee kutumia elimu waliyoipata kupitia Tasaf, kujenga uchumi wa familia na Taifa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana amesema Daraja la JP Magufuli linarahisisha usafirishaji wa bidhaa ambapo wajasiriamali wanaweza kwenda na kurudi, hasa kwa mikoa jirani kama Geita.
Akizungumzia Shule ya Sekondari Igogwe, Mama Pinda amesema mazingira bora huongeza ari ya mwanafunzi wa kike kusoma na kupunguza utoro unaochangiwa na umbali na vishawishi njiani.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimanirwentemi, Rutu Mikomangwa amesema ujenzi wa shule hiyo ulifanikiwa kwa ushirikiano kati ya mitaa minne na Tasaf.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Uswege Mwakalobo amesema ujenzi uligharimu zaidi ya Sh890 milioni na umepunguza changamoto ya wanafunzi kutembea zaidi ya kilomita saba kwenda shule za jirani.
Amesema tangu shule hiyo ianze, hakuna taarifa za ujauzito kwa wanafunzi na kuwa changamoto ipo kwenye bwalo la chakula na uzio.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 700, zaidi ya 80 wakihudumiwa na Tasaf.
Mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo, Samia Issa amesema maabara zilizopo zimewapa motisha ya kusoma sayansi na kuongeza ufaulu.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shadrack Mziray, Mkurugenzi wa Mfumo na Mawasiliano, Japhet Boaz amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuzingatia ombi la bwalo na uzio.
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Mwanza, Monica Mahundi amesema asilimia 92 ya walengwa katika mkoa huo hupata milo miwili hadi mitatu kwa siku, huku walengwa 38,804 wakianzisha miradi ya kiuchumi.
Amesema kaya 9,676 zimeboresha makazi, mahudhurio ya shule na kliniki yameongezeka kwa asilimia 95 na wanafunzi 106 kutoka kaya masikini wamejiunga na vyuo vikuu.
Amesema watoto 39,567 wanatimiza masharti ya elimu na afya kupitia ruzuku.