Wasiwasi bei ya mafuta ikipaa soko la dunia
Muktasari:
- Bei ya mafuta duniani imevuka Dola 100 (takribani TSh 270,000) kwa pipa kutokana na mvutano wa Mashariki ya Kati.
Dar es Salaam. Bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia imevuka Dola 100 (takribani Sh 270,000) kwa pipa kwa mara ya kwanza ndani ya miezi miwili, kufuatia kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi Mashariki ya Kati unaotishia usafirishaji wa mafuta kupitia Bahari ya Shamu (Red Sea).
Hali hiyo inazua wasiwasi kuhusu ongezeko la gharama za nishati na mfumuko wa bei duniani, ikiwemo Tanzania.
Kulingana na Shirika la Habari la Al Jazeera na The New York Times, mafuta ghafi aina ya Brent, ambayo hutumika kama kipimo cha kimataifa cha bei ya mafuta, yamefikia Dola 100.64 (takribani TSh 271,728) kwa pipa jana Alhamisi, Julai 23, 2026, ikiwa ni ongezeko la Dola 6.57 (takribani TSh 17,739), sawa na asilimia saba.
Kwa upande wa mafuta aina ya West Texas Intermediate (WTI), yanayotumika kama kipimo cha soko la Marekani, bei imepanda hadi Dola 91.83 (takribani TSh 247,941) kwa pipa, sawa na ongezeko la asilimia 5.8.
Hii ni mara ya kwanza bei ya Brent kuvuka kiwango cha Dola 100 (takribani TSh 270,000) kwa pipa tangu miezi miwili iliyopita, huku wachambuzi wakihusisha ongezeko hilo na kuzorota kwa hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ongezeko hilo limechochewa na mashambulizi mapya yaliyodaiwa kufanywa na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran dhidi ya meli mbili za kubeba mafuta za Saudi Arabia zilizokuwa zikisafiri katika Bahari ya Shamu.
Mashambulizi hayo yameongeza hofu kuhusu usalama wa Mlango wa Bahari wa Bab el-Mandeb, njia muhimu inayounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, ambayo hupitisha takribani asilimia saba ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.
Waasi wa Houthi wametangaza mpango wa kuanzisha kile walichokiita kuizingira bahari dhidi ya Saudi Arabia katika eneo hilo, hatua inayoongeza hofu ya kusambaratika kwa mnyororo wa usafirishaji wa mafuta duniani.
Kupanda kwa bei ya mafuta pia kumekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuionya Iran kuwa itawajibishwa moja kwa moja endapo kutakuwa na mashambulizi zaidi ya Houthi dhidi ya meli zinazopita Bahari ya Shamu.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump amewashutumu waasi hao kwa kushambulia meli mbili za Saudi Arabia na kuonya kuwa Marekani iko tayari kutoa "adhabu kubwa ya kijeshi" dhidi ya Iran na Houthi.
Kupanda kwa bei ya mafuta tayari kumeanza kuathiri masoko ya fedha duniani, huku wawekezaji wakihofia kurejea kwa kasi kwa mfumuko wa bei.
Nchini Marekani, wastani wa bei ya petroli umeongezeka hadi Dola 4.09 (takribani TSh 11,043) kwa galoni, kutoka Dola 3.94 (takribani TSh 10,638) wiki moja iliyopita.
Masoko ya hisa pia yameguswa na hali hiyo, ambapo fahirisi ya S&P 500 na Dow Jones Industrial Average zilishuka kwa takribani asilimia moja, huku Nasdaq Composite ikiporomoka kwa asilimia 1.8.
Katika soko la London, fahirisi ya FTSE 100 ilishuka kwa asilimia 0.96 hadi pointi 10,613.61 kutokana na hofu ya kupanda kwa gharama za nishati.
Hata hivyo, kampuni kubwa za mafuta zimenufaika na hali hiyo, huku hisa za Shell zikiongezeka kwa asilimia 1.4 na zile za BP kwa asilimia 2.6 kutokana na matarajio ya mapato makubwa yanayotokana na bei ya juu ya mafuta.
Kupanda kwa bei ya mafuta kumeongeza shinikizo kwa Benki Kuu ya Marekani (Fed), ambayo inatarajiwa kutangaza uamuzi wake kuhusu viwango vya riba mwishoni mwa mwezi huu.
Wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa gharama kubwa za nishati zinaweza kuongeza mfumuko wa bei na kuifanya Fed kusitisha mpango wake wa kupunguza viwango vya riba au hata kuongeza viwango hivyo ili kudhibiti shinikizo la bei.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya uwekezaji ya deVere Group, Nigel Green, amesema matarajio ya wawekezaji kuona viwango vya riba vikishushwa baadaye mwaka huu sasa yamepungua.
"Matarajio ya kupunguzwa kwa viwango vya riba ambayo wawekezaji walikuwa wakiyategemea sasa hayana uhakika kama ilivyokuwa hata wiki moja iliyopita," amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za CME FedWatch, uwezekano wa Fed kuongeza kiwango cha riba katika kikao chake kijacho umeongezeka hadi asilimia 36 kutoka asilimia 11 wiki moja iliyopita.
Wataalamu wa Oxford Economics wamesema uwezekano wa usumbufu wa usafirishaji wa mafuta kupitia Bahari ya Shamu unaendelea kuongezeka, wakitabiri bei ya mafuta inaweza kubaki juu ya Dola 85 (takribani TSh 229,500) kwa pipa kwa kipindi chote kilichobaki cha mwaka.
Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji wa kampuni ya Killik & Co, Lucy Smith, amesema ongezeko hilo linaonyesha jinsi migogoro ya kisiasa duniani inavyoweza kuathiri haraka soko la nishati.
Amesema ingawa kupanda kwa sasa kunachochewa zaidi na mashambulizi ya Houthi kuliko upungufu mkubwa wa mafuta sokoni, hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo mashambulizi yataongezeka katika njia muhimu za usafirishaji au miundombinu ya nishati.