Wakulima wapigwa butwaa bei ya mahindi kushuka ghafla

Muktasari:
- Irine Nahaonga, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Sumbaluwela, Kata ya Ihanda, wilayani Mbozi, ameiambia Mwananchi Digital kuwa amestaajabishwa na kushuka kwa bei ya mahindi kutoka Sh85000 hadi 66,000 kwa gunia la kilo 100
Songwe. Bei ya mahindi katika masoko mbalimbali katika Mkoa wa Songwe imeporomoka katika kipindi cha mwezi mmoja ikilinganisha na bei zilizokuwepo mwezi Juni na Julai mwaka huu.
Irine Nahaonga, Mkulima na Mkazi wa Kijiji cha Sumbaluwela, Kata ya Ihanda, wilayani Mbozi, ameiambia Mwananchi Digital kuwa amestaajabishwa na kushuka kwa bei ya mahindi kutoka Sh85000 hadi 66,000 kwa gunia la kilo 100.
"Wanunuzi wenye stoo, wametaka wanunue mahindi yangu kwa bei ya Sh66, 000 badala ya Sh85, 000 niliyokuwa nimeitarajia awali," amesema mkulima huyo aliyepeleka mahindi yake sokoni.
Aidha katika kipindi cha mwezi Juni na Julai mwaka huu, mahindi yalikuwa yakiuzwa kwa bei ya kati ya Sh80, 000 na Sh84, 000 kwa gunia lenye ujazo huo.
Katika soko la mazao Mlowo, wilayani Mbozi, Tumaini Enson, amesema kushuka kwa bei hizo mwezi Agosti, kunatokana na wanunuzi kutofika, jambo lililosababisha kuwa na mahindi mengi na bei kushuka.
"Kuanzia juzi walau bei imeanza kuongezeka kidogo kutoka Sh66, 000 hadi Sh72, 000 siku ya leo, hivyo kuna nafuu kidogo,” amesema Tumaini.
Meneja wa Soko la Kimataifa la Mazao Katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Edward Silwimba, amesema sokoni kwake bei ya mahindi kwa gunia ni kati ya Sh72, 000 na Sh78, 000.
Silwimba amekiri kuwa, kukosekana kwa wanunuzi kumechangia hali hiyo japo ana matumaini kwani sasa wanunuzi wameanza kufika sokoni hapo.
Kwa upande wake Johnson Kayange, Mkazi wa Ihanda, analaumu kuyumba kwa bei ya mahindi akisema: “...kipato kupunguza sana, tukienda kuuza, tunapata fedha kidogo ukilinganisha na siku za nyuma bei zilipokuwa juu.”
Hata hivyo bado anakiri kuwa, japo bei ni ndogo, haziwezi kulinganishwa bei za kuanzia 2019 kurudi nyuma, kwani kipindi hicho, gunia la kilo 100, liliuzwa kati ya Sh36, 000 na Sh42, 000.
Kutoka Kijiji cha Itaka wilayani Mbozi, mkazi wa Kijiji hicho Aida Mwasenga, amesema wanunuzi kutoka maeneo ya mjini wanafika kijijini hapo na kununua mahindi kwa bei ndogo ya kati ya Sh54000 na 60000 kwa gunia.
Ili kupata kauli ya Serikali, Mwananchi Digital imewatafuta viongozi wakuu wa Wizara ya Kilimo, ambao ni pamoja na Waziri Hussein Bashe, naibu wake Davidi Silinde, na Katibu Mkuu Gerald Mweli, hata hivyo simu zao ziliita bila majibu.
Mwananchi Digital ilitaka kujua kama kushuka kwa bei hizo kunatokana na kauli ya Serikali inayotaka kufuatwa kwa taratibu za uuzaji mazao yakiwemo ya chakula nje ya nchi.
Utaratibu huo kwa mujibu wa Bashe kama alivyowahi kunukuliwa mwezi June mwaka huu, ni pamoja na mfanyabiashara ni kusajili kampuni yake hapa nchini, awe amekata leseni ya kusafirisha mazao nje ya nchi, awe na namba ya utambulisho ya mlipakodi (TIN) na awe na leseni ya biashara.
Lakini pia Serikali ilipiga marufuku kwa wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi, kununua mazao na kuyasafirisha kwa leseni za biashara za madalali wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Wazir Bashe, utaratibu huo unalenga kuongeza eneo la ukusanyaji wa kodi na kuhakikisha wanawarasimisha wauzaji wa nafaka nje.
"Tunataka wasafirishaji wa mazao nje waanze kupokea malipo kwa njia ya benki, haiwezekani tuuze mahindi moja ya nchi jirani tani 400,000 zaidi ya Sh300 bilioni halafu haionekani kwenye mfumo wa benki,” amesema wazir huyo.
Hata hivyo, Julai 13, mwaka huu akiwa mkoani Mwanza, Rais Samia Suluhu Hassan alishauri wakulima wasiuze mazao ya chakula nje ya nchi, badala yake waiuzie Serikali ili iongeze hifadhi ya ndani. Kauli yake hiyo inatokana na kile alichoeleza kuna viashiria vya dunia kukabiliwa na njaa kwa siku zijazo
“Kwa sasa nchi ina akiba ya chakula tani 200,000 hadi 250,000, tuna mpango wa kumwaga fedha kununua chakula, tunataka kuwa na hifadhi ya chakula tani 500,000 kwa mwaka huu tunaouanza, hivyo msiuze mazao nje kwa kuwa Serikali itayanunua," alisema Rais Samia.